Ofisa Mradi anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Utawala wa
Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Michael Nilonga
akizungumza na waandishi kuhusu Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya
Mkaa Tanzania (TTCS) ulivyosaidia wana Vijiji zaidi ya 800 kupata Hati
za Hakimili za Kimila wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Na Suleman Msuya
Na Suleman Msuya
WILAYA ya Kilosa
imepanga kutumia uzoefu wa uhifadhi wa misitu katika vijiji 20 vilivyopo kwenye
Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), kuendeleza Usimamizi
Shirikishi wa Misitu (USM) wilayani humo.
Vijiji 20
vinavyotekeleza mradi wa TTCS unaohimiza USM, ilioanza kutekelezwa mwaka 2012
chini ya Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa
Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania (TaTEDO) kupitia ufadhili wa Shirika
la Maendeleo la Uswis (SDC) umechochea uhifadhi katika vijiji hivyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya hiyo Adam Mgoi, alisema
mradi wa TTCS umeweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya misitu na
mazingira jambo ambalo limechangiwa na uwepo wa mpango wa USM.
Mgoi alisema Kilosa
ilikuwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira kutokana na uwepo wa
rasilimali nyingi za misitu isiyosimamiwa vizuri lakini baada ya mradi kuja
umefanikisha kuwepo mpango mzuri wa matumizi ya ardhi na uvunaji msitu.
“TTCS imefanikisha USM
kuwepo wilayani kwetu katika vijiji 20 hivyo tunaahidi kusamba elimu hiyo
katika vijiji 119 vilivyobakia ili siku moja Kilosa ile ya miaka ya nyuma iweze
kurejea na mazingira kuwa rafiki.
Kwa sasa mpango wa
ukataji miti kiholela haupo, lakini pia ipo fursa ya miti mingine kuweza kuota
katika maeneo ambayo awali yalikuwa yanakabiliwa na uharibifu,” alisema.
Mgoi alisema pamoja na
uhifadhi kuongeza vijiji, halmashauri na wanavijiji wamekuwa wakinufaika na
rasilimali mizitu jambo ambalo linawasukuma kusamba mradi huo ili kunufaisha
jamii ya Kilosa.
Mkuu wa wilaya alisema
pia wamenufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi hivyo kumaliza migogoro
baina ya wakulima, wafugaji na wananchi wengine.
“Halmashauri
tumejipanga kuhakikisha kwamba hili linakuwa la vijiji vyote 139 vilivyopo ambapo
wataalam wetu watapatiwa fedha na halmashauri kuanza utekelezaji, lakini bado
tunaomba mradi utuangalie katika awamu ya tatu tupate vijiji vingine,” alisema.
Mgoi alitoa wito kwa
wananchi wa Kilosa ambao wamefanikiwa kupata Hati za Hakimiliki za Kimila
kuzitumia kwa ajili ya kujiongezea kipato kwa kuchukua mikopo kwenye taasisi za
fedha na pia zitumike kuondoa migogoro ambayo imekuwa kwa muda mrefu.
Akizungumzia mradi huo
Mtendaji wa Kijiji cha Madizini kata ya Kisanga, Cosmas Tayari alisema kijiji awali
kilikuwa na migogoro mingi ya ardhi lakini ujio wa TTCS umeweza kumaliza
migogoro.
“Mradi huu ni fursa ambapo
wananchi wamepata elimu ya kutosha kuhusu uhifadhi wa misitu endelevu na
upimaji wa ardhi ambapo zaidi ya wananchi 200 wamepatiwa hati za hakimiliki za
kimila ni wazi thamani ya ardhi itaongezeka,” alisema.
Ofisa Mradi
anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Utawala kutoka TFCG, Michael Nilonga
alisema katika vijiji 20 vya Kilosa wamefanikiwa kutoa hati za hakimiliki za
kimila kwa wanavijiji zaidi ya 800 katika vijiji vitano vya Kigunga (62), Nyali
(200), Madizini (200), Dodoma Isanga (200), Ulaya Mbuyuni (125)
Alisema wanatoa
vipambele kwa familia ambazo zina kipato kidogo, zenye mzazi mmoja hasa wakina
mama na wahitaji kwa kuzingatia vigezo vya umiliki na kuepuka maeneo yenye
migogoro.
Nilonga alisema ili
kikijiji kipate hati za hakimiliki za kimila ni lazima kiwe vigezo vitatu
ambavyo ni cheti cha kijiji, mpango wa matumizi bora ya ardhi na masijala ya
ardhi hivyo kuiomba Halmashauri ya Kilosa kuongeza kasi ya utoaji wav yeti vya
vijiji.
Wanavijiji wa Kijiji
cha Madizini William Mwinge, Anthony Pacific, Joanitha Kiwanga na Joram Mahiwa, Agnes
Mathius na Mwanaharusi Athuman wa Kijiji cha Nyali wamesema mradi wa TTTCS
umeweza kuwakomba kimaisha, kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment