HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 06, 2019

Matamko kandamizi yachangia kuporomoka kwa uhuru wa habari

NA BETTY KANGONGA
  
MATAMKO endelevu yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali yamekuwa chanzo cha kukandamiza Uhuru wa habari nchini.
 
Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakitoa matamko yanayovunja sheria na kukandamiza Uhuru wa kujieleza nchini jambo linalozidisha hofu miongoni mwa jamii.
 
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dodoma, Mratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) William Mtwazi, alisema kuwa matamko hayo hayazingatii viwango na weledi katika ufanisi wa kazi zao.
 
Mtwazi alisema, matamko hayo yanaleta hofu kwa Watanzania na watumishi wa ngazi za chini jambo linaloleta sintofahamu katika uhuru wa habari.
 
"Kuna hofu pia inayojengwa na vyombo vya dola unakuta wanahabari wanakamatwa na kuswekwa ndani pasipo kupandishwa mahakamani hali hii inatoa taswira mbaya katika uhuru wa habari nchini," alisema Mtwazi.
 
Alitaja suala jingine linaloonyesha kuminywa kwa uhuru wa habari ni pamoja na wanasiasa kushindwa kufanya shughuli zao kwa uhuru.
 
Akitolea mfano Mtwazi alisema, wapo baadhi ya wanasiasa anafanya kazi zao Kihalali lakini ghafla anakamatwa na kuswekwa ndani.
 
Alisema kuwa masuala hayo yamekuwa chanzo cha kuporomoka kwa uhuru wa habari nchini.
 
"Wanaharakati nao kwa sasa hawapo huru wanapofanya kazi zao kwa halali wanajikuta wakikamatwa na kutakiwa kuacha kufanya utetezi wowote hivyo nimejikuta wakishindwa kutekeleza majukumu yao na matokeo yake wamejaa hofu," alisema.
 
Mtwazi alisema kuwa hali hiyo inachangia kushuka kwa kiwango cha uhuru wa habari Tanzania.
Mratibu huyo alisema, kuwa maendeleo yoyote hayawezi upatikanaji iwapo serikali itashindwa kuzingatia uhuru wa habari nchini.
 
"Tunataka kujenga Tanzania ya viwanda, sasa tutawezaje kufanikiwa kama tunaminya sauti za watu hivyo hatutaweza kufanikiwa kama kuna kundi katika jamii litakosa fursa ya kutoa michango yao," alisema.
 
Pia Mtwazi aliwataka wanahabari kuhakikisha wanatumia kalamu zao na kukemea pindi wanapoona ukiukwaji wa haki za binadamu ukiminywa.
 
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria semina hiyo walisema kuwa, utungwaji wa utungwaji wa baadhi ya sheria mbalimbali ikiwemo ya takwimu na ile ya makosa ya mtandao imechangia kuminya kwa uhuru wa habari kwa vyombo vya habari hivyo vyombo hivyo vimejikuta vikipangiwa nini cha kuripoti hatua inayoashiria ni sawa na kuviziba mdomo.

No comments:

Post a Comment

Pages