Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto wa Tanzania, Ummy Mwalimu.
Na Suleiman Msuya
MAWAZIRI
wanaosimamia sekta za Afya na Ukimwi katika nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wameazimia kuanzisha kikosi kazi cha
uratibu wa pamoja kushughulikia ugonjwa wa Ebola.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto wa Tanzania, Ummy Mwalimu wakati akitoa maazimio matano ya
mkutano wa mawaziri wa sekta hiyo walikutana jana jijini Dar es Salaam.
Mwalimu
ambaye ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Sekta hiyo ya Afya na Ukimwi kwa
nchi za SADC, alisema uamuzi wa kuanzisha kikosi kazi umejikita katika
kukabiliana na maafa na magonjwa ya dharura yanayotokea kwa mara katika
nchi wanachama.
"Jana
tumekaa na kujadiliana ambapo tumetoka na maazimio matano moja ya wapo
ni hili la maafa na dharura ambalo litahusisha uanzishaji wa kikosi kazi
cha uratibu wa pamoja wa kushughulikia ugonjwa wa Ebola Afrika,"
alisema.
Mwalimu alisema
wamekubaliana kuboresha mafunzo kuhusu masuala ya maafa na dharura,
kushirikiana katika maandalizi ya mwitikio wa dharura ikiwemo kuwajengea
uwezo kwa watoa huduma katika maeneo ya mipaka na kupeana taarifa kwa
wakati.
Aidha, Waziri
Mwalimu alisema katika kukabiliana na changamoto ya lishe kwa nchi
wanachama wanatarajia kuanzisha matumizi ya kadi alama za lishe na
kuweka kanuni za pamoja za katazo la uhamasishaji wa matumizi ya maziwa
ya kopo na vyakula mbadala kwa watoto wachanga na wadogo na kumlinda
mama anayenyonyesha (likizo ya uzazi).
“Tumeweka
kanuni za pamoja za katazo la uhamasishaji wa matumizi ya maziwa ya
kopo na vyakula mbadala kwa watoto wachanga na wadogo na kumlinda mama
anayenyonyesha yaani likizo ya uzazi,” alisema.
Alisema
watoto wengi wanashindwa kunyonya kwa kipindi wanachohitaji kiasi
kwamba wanaanzishiwa maziwa mbadala mapema jambo ambalo ni kinyume na
kanuni za afya.
Alisema
wameazimia kutumia mfumo wa kikanda kuboresha lishe kwa watoto na
mkakati wa kikanda wa kudhibiti uzito uliozidi na kiribatumbo katika
jamii.
Pia Mwenyekiti
huyo alisema azimio hilo linataka uongwezwaji wa virutubishi vya
vitamini na madini wakati wa usindikaji kwenye unga wa mahindi, unga wa
ngano, sukari, mafuta ya kula na chumvi.
Kuhusu
azimio la malaria Mwalimu alisema kutokana na ugonjwa huo kuendelea
kuwa tishio wameazimia kuendelea kufuatilia ubora wa dawa za kutibu
malaria na kufanya utafiti wa usugu wa vimelea vya malaria dhidi ya dawa
zinazotumika.
Alisema
pia wataendeleza mapambano dhidi ya malaria katika nchi za SADC na
kuendelea kufuatilia ubora wa viuatilifu vinavyotumika kwenye afua za
vyandarua na dawa ukoko ili kuona kama vinaendelea kuwa na ubora
unatakiwa katika kudhibiti mbu na kuendelea na utafiti ili kubaini
maeneo yenye maambukizi makubwa.
Mwenyekiti
huyo wa baraza la mawaziri wa afya na Ukimwi SADC alisema
wamekubaliana kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa
kuweka kipaumbele katika kutoa huduma za unahisi na kupima kwa makundi
yakiyoko katika hatari ya kuambukizwa ikiwemo vijana balehe wa kike na
kina mama wadogo.
"Nchi wanachama watajikita katika matumizi ya dawa ili kufikia malengo ya 90,90,90 ya kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030," alisema.
Waziri
Mwalimu alitaja azimio la tano ni kuhusu Kifua Kikuu (TB) ambapo nchi
za SADC zinachangia asilimia 77 ya wagonjwa katika Bara la Afrika.
Alisema
wamepitisha mpango wa 2020 hadi 2025 ili kuhakikisha ifikapo 2030 kifua
kikuu hakipo na kushirikiana, kuoanisha sera na miongozo ya kitaifa ya
kudhibiti TB katika ukanda wa SADC.
Pia
wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya mipango ya TB na Ukimwi,
sekta binafsi, asasi za kiraia na sekta nyingine katika ukanda.
"Pia
tumeimarishe udhibiti wa TB migodini hasa wachimbaji wa madini kwenye
mipaka kwa kuboresha mifumo ya utoaji wa taarufi na rufaa ya wagonjwa wa
nchi wanachama," alisema.
No comments:
Post a Comment