Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof. Zacharia Mganilwa, akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya madereva wa
mabasi wanawake katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
NA TATU MOHAMED
WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema
kuwepo kwa madereva wengi wanawake kutaenda kuwa muarobaini wa ajali
nchini kutokana na umakini wao wawapo barabarani.
Waziri
Kamwelwe ameyasema hayo wakati wa kufungua mafunzo ya madereva wa
mabasi wanawake katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo
amesema endapo madereva wengi wa mabasi wangekuwa wanawake
kusingekuwepo kwa ajali za barabarani za mara kwa mara .
Amesema,
mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuwa na wanawake 100 yamekuja wakati
muafaka kwani serikali inatelekeza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kufikia
uchumi wa viwanda ifikapo 2025 kwa kujenga miundombinu mbalimbali.
‘’Tunaamini
wanawake wataboresha usalama wa usafiri kwa maendeleo endelevu. Mtumie
elimu mtakayopata kulinda rasilimali za watanzania zilizopatikana
kupitia kodi zao kwa sababu tunaamini mtapata ajira katika taasisi
mbalimbali,’’ amesema Kamwelwe.
Ameongeza
kuwa watahakikisha wanasogeza mafunzo hayo katika Mikoa ya Arusha,
Mwanza na Mbeya ili wanawake wengi waweze kufundishwa udereva wa mabasi
na magari makubwa.
Naye,
Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema watatoa mafunzo
kwa madereva hao kati ya 300 walioomba mafunzo hayo ambapo baada ya
kukamilika kwa wiki saba watafanikiwa kupata leseni ya daraja C
itakayowapa fursa ya kuendesha magari ya abiria.
Amesema
wameweka mkakati wa kuanzisha kitengo cha mafunzo ya usalama barabarani
ikiwemo kutoa wataalamu wa mizani ili kusaidia Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini
(LATRA), Gilliard Ngewe amesema ajali nyingi za barabarani zinazotokea
kwa asilimia 76 hadi 80 husababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwemo
madereva.
Kwa upande
wake, Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus
Musilimu amesema wanaamini ajira nyingi zitapatikana kwa madereva hao
wanawake baada ya mafunzo hayo.
Amesema
madereva hao watahangia ukuaji wa uchumi wa kati kwa kusafirisha
malighafi mbalimbali zitakazozalishwa kupitia viwanda vilivyopo na
kwamba watasaidia kuboresha usalama barabarani.
‘’Takwimu
za ajali kati ya wanawake na wanaume kwa kipindi cha Januari hadi
Septemba 2019 zilikuwa 110 na kati ya hizo madereva wanaume 109
walipoteza maisha huku kukiwepo kifo kimoja kwa dereva wa kike. Upande
wa majeruhi ni madereva 209 kati yao 182 wanaume na wanawake ni 27,’’
alisisitiza.
Kwa mujibu wa Musilimu, wanawake wapo makini barabarani na ni kundi ambalo liko salama katika masuala ya ajali barabarani.
No comments:
Post a Comment