Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya siku
16 za kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa
katika picha ya pamoja wanafunzi wa moja ya shule ya Sekondari ya Dodoma mara
baada ya uzinduzi wa siku 16 za Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia
iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WAMJW).
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewaagiza Maafisa
Maendeleo ya Jamii kusimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa Kamati za ulinzi wa
wanawake na watoto katika mikoa na Halmashauri ambazo hazijaanzishwa ili kuzuia
vitendo vya ukatili wa kijinsia hadi ngazi ya Kata na Vijiji.
Akizungumza katika
uzinduzi wa Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsi leo Jijini Dodoma,
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu amesema
kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe
Magufuli imetekeleza kwa vitendo azma ya kukomesha vitendo hivyo.
Waziri Ummy ameongeza
kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na asasi za Kiraia katika mapambano dhidi
ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika maeneo yote hapa nchini.
Aidha, Mhe Ummy
ameagiza kuanzishwa kwa Madawati ya Jinsia Katika Taasisi za Elimu ya Juu ili
kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono na ukatili mwingine kwa wanafunzi wa vyuo
vya elimu ya juu.
Aliongeza kuwa kuanzishwa
kwa madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi yapatayo 420 yamewezesha
wahanga 58,059 kuripoti aina mbalimbali za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa rika
mbalimbali wakiwemo watu wazima na watoto katika matukio ya ubakaji, ulawiti,
vipigo na ukeketaji.
Akizungumzia faida za
madawti hayo Waziri amesema kuwa yameongeza mwamko wa wananchi katika kujiamini
na kutoa taarifa za ukatilii unapotokea kwenye maeneo yao.
Kuongeza vituo vya
Mkono kwa Mkono vya Kutoa huduma kwa
wahanga wa ukatili wa Kijinsia (One Stop Centres) kutoka vituo 10 mwaka 2017
hadi 13 mwaka 2019 ili kiwezesha utoaji wa huduma rafiki na kwa haraka kwa wahanga. Hatua hiyo inapelekea Serikali
ya Awamu ya Tano kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza Mpango
wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/2018- 2021/2022
ambao unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika
Jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Kauli mbiu ya Kampeni
ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu ni “Kizazi chenye Usawa:
Simama Dhidi ya Ubakaji” kauli mbiu hii inawapa jukumu wananchi wote kutafakari
wajibu wao kama kizazi kinachoamini na kuthamini usawa wa kijinsia.
Kauli mbiu hii inatoa
msukumo wa kuhakikisha kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na kuchukua
hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kingono hasa ubakaji
na matendo yote ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali
ikiwemo katika nyumba na mahali pa kazi na katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule
na vyuo mbalimbali.
Aidha, Serikali
inapinga vikali mila, desturi na imani zote zenye madhara kwa jamii kama
ukeketaji, kukatisha watoto wa kike shule kwa ajili ya kuolewa.
Kwa upande wake
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake Bi
Hodan Addou amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya
Tanzania kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia kwa makundi yote ili kujenga
jamii yenye usawa.
Pia alipongeza juhudi
za Serikali katika kuhakikisha inakomesha vitendo hivyo kupitia mpango mkakati
wake na kuahidi kuendelea kuunga mkono
juhudi hizo.
Aliongeza kuwa
vitendo vya ukatili wa kijinsia ni tatizo la kidunia linalohitaji jitihada za
pamoja katika kulikomesha.
Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
umefanyika Jijini Dodoma na umefanywa na
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na kuhudhudhuriwa na
Asasi zisizo za kiserikali, viongozi wa Serikali, Mashirika ya Umma pamoja na
Viongozi wa Dini.
No comments:
Post a Comment