HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 11, 2019

WAZIRI WA KILIMO MHE HASUNGA APIGA MARUFUKU BIASHARA YA RUMBESA NCHINI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mashamba ya kilimo cha mahindi wakati akiwa katika ziara ya kikazi kijijini Mang'ola katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha jana tarehe 10 Novemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Sehemu ya wakazi wa Kijiji cha Mang'ola wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akiwa katika ziara ya kikazi kijijini Mang'ola katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha jana tarehe 10 Novemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Karatu wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Arusha tarehe 10 Novemba 2019. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo kukagua mashamba ya kilimo cha mahindi wakati akiwa katika ziara ya kikazi kijijini Mang'ola katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha jana tarehe 10 Novemba 2019. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Karatu
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana tarehe 11 Novemba 2019 amewataka wakuu wa mikoa yote nchini kwa kushirikiana na kamati za ulinzi za mikoa na wilaya kuwakamata wafanyabiashara wote nchini wanaonunua mazao kwa wakulima kwa njia ya Rumbesa.
Ametoa agizo hilo wakati akiwa katika ziara ya kikazi linalohusisha vipimo vya ujazo wa mazao ikiwemo kupiga marufuku ujazaji wa rumbesa na mizani isiyotenda haki kwa wakulima.
Alisema kuwa Rumbesa, na mizani isiyokuwa ya haki kwa wakulima ni kosa kisheria, hivyo kamati za siasa za mikoa, wilaya, kata na matawi zinapaswa kusimamia jambo hilo na kuwataka kutoa taarifa ili wananchi wanyonge wasiendelee kunyanyasika.

Wakizungumza kwenye mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Kilimo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo, wakulima wa Kijiji cha Mang’ola wamesema kuwa mifuko inayotumika kufungashia vituguu inakuwa na ujazo mkubwa kuanzia kilo 120 hadi 180  wakati wa kuwapimia wafanyabiashara.

Aidha, wamesema kuwa gharama za uzalishaji zimekuwa juu hivyo kwa kuuza vitunguu au mazao mengine kwa rumbesa kunawatia hasara na kushindwa kurudisha gharama za uzalishaji jambo ambalo limewafanya kuiomba serikali kuingilia kati.

Katika hatua nyingine Mhe Hasunga ameiagiza Tume ya umwagiliaji nchini kufika katika eneo maalumu la kilimo cha vitunguu Mang'ola katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha  kubaini maeneo ya kuchimba visima vya maji ili wakulima waweze kunufaika na kilimo.“Kuna haja ya kujenga mabwawa na kuweka kingo za kuzuia maji ili kuimarisha sekta ya kilimo nchini” Alisisitiza

Amewahakikishia wakulima hao kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wizara ya Maji, Wizara ya nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEM) pamoja na Halmashauri za wilaya itaweka mkakati madhubuti wa kuwasaidia wakulima ili waweze kuzalisha mazao ya kilimo katika kipindi cha mwaka mzima tofauti na kufanya kilimo cha kutegemea msimu wa mvua ambao ni mara moja kwa mwaka.

Pia ametoa mwito kwa wadau wa sekta ya kilimo na maendeleo kujitokeza kwa ajili ya kuchimba visima na mabwawa yatakayonusuru upotevu wa maji katika wilaya ya Karatu.

No comments:

Post a Comment

Pages