Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard
Konga akiongea na Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu masuala
mbalimbali ya mfuko huo, Leo 02/12/2019 Jijini Dar es Salaam. (Picha na Maelezo).
Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya
(NHIF) Bw. Christopher Mapunda akiwasilisha mada kwa Wahariri wa vyombo
vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya mfuko na kuanzishwa kwa
vifurushi via Bima ya Afya, Leo 02/12/2019 Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wakisikiliza
uwasilishaji wa mada mbalimbali kuhusu Maendeleo ya Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya na uanzishwaji wa Vifurushi vya Bima ya Afya.
Na Mwandishi Wetu
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema upo imara na unaweza kujiendesha na kutoa huduma kwa wanachama wake hadi mwaka 2024 bila kupokea michango yoyote kutoka kwa wanachama
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga kwenye mkutano
kati ya Mfuko na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari uliofanyika
Dar es Salaam leo, kuelezea manufaa ya mpango wa vifurushi vipya
“Naomba
niseme wazi kuwa Mfuko haujayumba wala kutetereka kifedha kama
inavyodaiwa, tathmini ya Uhai wa Mfuko inaonesha tunao uwezo wa
kuwahudumia wanachama wetu kuanzia sasa mpaka mwaka 2024 bila kupokea
michango yoyote kutoka kwa wanachama, hivyo madai yanayoenezwa sio ya
ukweli,” alisema Bw. Konga.
Alisema
kuwa madai ya ucheleweshaji wa kulipa madai kwa baadhi ya watoa huduma
hayatokani na kukosa fedha za kulipa bali inatokana na sababu mbalimbali
ikiwemo kujiridhisha kwa madai hayo.
“Kuna
sababu nyingi za kuchelewesha madai, yapo madai yanakuja na viashiria
vya udanganyifu hayo huwezi ukalipa mapema ni lazima uhakikishe
umejiridhisha ili ulipe fedha halali na ulinde fedha za wanachama
zisitumike isivyo halali,” alisisitiza Bw. Konga.
Akizungumzia
uanzishwaji wa vifurushi vipya, alisema kuwa vifurushi hivyo vina lengo
la kuwahakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu wananchi wote
watakaojiunga na mpango huo.
Alisema
kuwa vifurushi hivyo vimebeba huduma zote za matibabu ya msingi ambayo
mwananchi aliyejiunga na vifurushi hivyo ana uwezo wa kupata huduma za
matibabu katika vituo vyote vilivyosajiliwa na Mfuko Tanzania Bara na
Zanzibar.
“Mfuko
haujabuni vifurushi hivi kwa lengo la kuongeza mapato ya Mfuko.
Vifurushi ni kwa ajili ya kifikia watanzania wengi walio katika sekta
binafsi ambao hawana fursa yoyote ya kupata bima binafsi hivyo niwatoe
wasi wasi wananchi juu ya mpango huu, ni mpango ambao una manufaa kwa
ajili ya afya za wananchi,” alisema Bw. Konga.
No comments:
Post a Comment