HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 07, 2019

NYOTA WA KIGENI YANGA WACHAFUA HALI YA HEWA

WAKATI Kocha Mwinyi Zahera akihaha kulipwa madai yake ya kuvunjiwa mkataba, baadhi ya nyota wa kigeni wa Yanga wameripotiwa kuandikia uongozi barua za kuvunja mikataba yao kwa kile walichokiita ‘uongozi kutoiheshimu mikataba hiyo’ kwa kutowalipa mishahara na stahiki zao nyingine kwa zaidi ya miezi mitatu.

Beki mahiri wa klabu hiyo, raia wa Ghana, Lamine Moro, alikuwa wa kwanza kabisa kuripotiwa kuwa amevunja mkataba wake baada ya Yanga kushindwa kumlipa mshahara wa miezi mitatu.

Hali hiyo, ilimsukuma Lamine, awasilishe kwa uongozi barua yake ya kuvunja mkataba wake na Yanga SC, lakini akaenda mbali zaidi kwa kuwasilisha barua hiyo kwa TFF na kutuma nakala ya barua hiyo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya FIFA.

Baada ya Lamine kufanya hivyo, kukaibuka wimbi la nyota wa kigeni kadhaa Yanga nao kufuata nyayo, wengi wakifanya hivyo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Yanga SC ilipanga kuwaondoa kundini baadhi ya wachezaji wa nje ambao wameonekana kuwa na viwango vya wastani ili kupisha wengine.

Imedaiwa kuwa, Yanga ilipanga ‘kuwachinja’ nyota hao ili kujipa nafasi ya kuongeza wengine katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo unaotarajia kuanza Desemba 15, 2019 hadi Januari 15 mwakani, huku ikitegemea nguvu ya tajiri mmoja ambaye jina lake liko mafichoni.

Kibopa huyo alikuwa tayari kuwalipa wachezaji hao sehemu ya gharama za kuvunja mikataba yao kwa maelewano maalum, lakini nyota hao wameshtuka na kuamua kuchukua hatua, sababu ya kutoaminiwa kwao ikitajwa kuwa ni kutowepo kwa Mwinyi Zahera aliyewasajili.

Ukiondoa Lamine Moro, nyota wengine wanaotajwa kuwemo kwenye sakata hili la kutaka kuondoka kwa kutokuheshimiwa mikataba yao ni pamoja Sadney Urkhob, David Molinga, Maybin Kalengo, Moustapha Seleman na Issa Bigirimana.

Jitihada za kuupata uongozi wa Yanga na TFF kuzungumzia sakata hili hazikuzaa matunda, lakini bado tunaendelea kuwasaka kusikia watasema nini juu ya mtanziko huo unaokinyemelea kikosi cha Charles Mkwasa.

No comments:

Post a Comment

Pages