Na Faraja Ezra
IMEELEZWA
kuwa ukuaji wa viwanda nchini hivi sasa umeongezeka zaidi kutoka
viwanda 513 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 542 mwaka 2019.
Aidha
ongezeko hilo linaleta hamasa kwa wadau mbali mbali wa biashara hasa
katika sekta binafsi na Umma kuweza kuwekeza zaidi katika bidhaa
zinazozalishwa ndani ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jani jijini Dar es Salaam katika kilele cha
maonesho ya nne ya viwanda nchini Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo Idara
ya Viwanda nchini Leo Lyayuka, alisema kiwango hicho kinakuza miundombinu ya biashara.
Alisema
ongezeko hilo ni juhudi zinazofanywa na wazalishaji na wanunuzi wa
ndani kuweka Ubunifu katika kuboresha bidhaa ili kuleta ushindani katika
soko la ajira ndani na nje ya nchi.
"Sisi
kama serikali tunayo jukumu la kuhakikisha sekta ya uchumi nchini
inakua kwa kiwango kikubwa ili kuendana na azma ya serikali ya uchumi wa
viwanda ifikapo mwaka 2025," alisema Lyayuka.
Hata
hivyo Lyayuka amewataka wadau mbalimbali wa biashara nchini kuweka
kipaumbele zaidi kwenye bidhaa za ndani lakini pia kuzalisha kwa wingi
na zenye ubora wa hali ya juu ili kuleta ushindani katika soko la
dunia.
Lyayuka alieleza
kuwa ili kuendana na soko la dunia ni lazima wazalishaji kuwa na
ubunifu katika kuzalisha bidhaa zenye ubora ili ziweze kupata soko kwa
haraka zaidi.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (Tantrade)
Edwin Rutageruka alisema maonyesho hayo yalianza rasmi disemba 5 hadi 9
mwaka 2019 yakilenga kuonesha bidhaa mbali mbali zinazozalishwa
nchini.
Alisema wadau
wa Tantrade wameweza kupiga hatua kubwa ya kibiashara kwa kuzalisha
bidhaa Bora na zenye kukubalika katika masoko mbali mbali duniani.
Pia kutokana na maonyesho hayo Rutageruka alisema wanunuzi wamevutiwa sana na kazi zao kwa kuwa na ubora wa hali ya juu.
Ametoa wito kwa wazalishaji kuendelea kuweka kipaumbele bidhaa za ndani pasi na bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.
" Tupende kutumia bidhaa zetu ili ziweze kuleta tija kwa wazawa wenyewe kabla ya kuwanufaisha wageni, " alisema Rutageruka.
No comments:
Post a Comment