HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 11, 2019

TPC WAANDAA SHINDANO LA UANDISHI WA MAKALA

Na Faraja Ezra

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limeandaa  shindano la uandishi wa  makala  katika maadhimisho ya miaka 40 ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) yanayotarajiwa kufanyika Januari 18 mwaka 2020 mkoani Arusha.

Aidha  maadhimisho hayo yameandaliwa na Shirika la posta Tanzania huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa ni Rais John Magufuli na pia kuhudhuriwa na Mawaziri  mbalimbali wa Mawasiliano Posta barani Afrika.

Umoja wa Posta Afrika PAPU ni taasisi ya mashirika ya posta kutoka kwenye kila nchi mwanachama  wa Umoja wa Afrika (AU).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam Meneja Mkuu Rasilimali za Shirika, Mwanaisha Said, alisema katika kuadhimisha  miaka 40 ya Umoja wa Posta Afrika kutakuwepo na matukio mbalimbali ikiwemo shindano la uandishi wa makala.

 Aidha Mwanaisha alisema  pia mada mbalimbali zimeandaliwa  ikiwamo makala kuhusu umuhimu wa anwani za Makazi na misimbo ya posta (postcode) katika kujenga Tanzania ya viwanda.

 Alisema ukubwa wa makala unatakiwa kuwa na maneno  kati ya 1000 hadi 2000 pamoja na kuonyesha  anwani  na e- mail na namba ya simu.

Baada ya makala kukamilika mwandishi atatakiwa kutuma  makala kwa njiavya EMS kwa anwani ya Meneja  masoko Shirika la posta Tanzania, jengo la "Posta house" Mtaa wa Ghana S.L.P 9551,11300 Dar es Salaam.

"Shindano hili litapelekea kuchaguliwa kwa washindi kumi pekee ambao makala zao ni bora zaidi na watapata zawadi mbalimbali zikiwamo komputa mpakato,  simu, smart phone, digital camera vyeti na fedha taslimu" alisema na kuongeza.

"Kwetu sisi hili ni shindano la kwanza kuwashirikisha waandishi  wa habari na tutaendelea kuimarisha ushirikiano huu kwani vyombo vya habari wamekuwa kiungo muhimu katika sekta ya posta," alisema Mwanaisha.

Pia kupitia vyombo mbali mbali wananchi na serikali wameweza kufahamu vyema  Shirika la posta kwa undani zaidi na kujua changamoto, Mipango na fursa  mbalimbali zilizoko ndani ya Shirika la posta Tanzania.

Mwanaisha ametoa wito kwa waandishi wa makala kutumia fursa hiyo ili kutoa hamasa kwa waandishi wengine ili kukuza tasnia ya habari kupitia makala mbalimbali lakini pia kukuza ushirikiano baina ya Shirika la posta na  vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment

Pages