HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 10, 2019

WAANDISHI WASHAURIWA KUJIUNGA JOWUTA

Na Mwandishi Wetu

WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kujiunga na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na kuanzisha matawi katika ofisi zao.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo kwa waandishi wa habari wanawake yaliyoandaliwa na chama hicho.

Alisema kwa miaka mingi waandishi wa habari wamekuwa wakipigania haki za watu wengine na kusaha za kwao hivyo wakati umefika kwa kujenga chombo sahihi kwa maslahi yao.

"Nitumie nafasi hii kuwaomba waandishi wa habari nchini kote kujiunga na JOWUTA ili tuwe na nguvu moja ya kupigania masalhi yetu kwani kwa muda mrefu tumekuwa tukipitia wakati mgumu sana," alisema.

Msuya alisema JOWUTA imejipanga kupita katika vyombo vya habari ili kuweza kuzungumza na wamiliki na waandishi kuhusu ushiriki wa pande zote kwa chama hicho.

Alisema vyama vya wafanyakazi ni takwa la kisheria hivyo mwajiri na mwajiriwa wanapaswa kulitekeleza kivitendo na sehemu sahihi ni JOWUTA.

Katibu huyo aliwataka waandishi wa habari kuanzisha matawi ndani ya vyombo vyao kwa kuwa hiyo ni haki yao ya kisheria.

Aidha, alisema taaluma ya habari imekuwa na changamoto ikilinganishwa na fani nyingine, ikiwamo ajira, usalama duni na kusababisha wengi wao kukosa haki za kustaafu kisheria hivyo JOWUTA wamejipanga kupigania hilo.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Simbarashe Msasanuri, wanahabari ili kubadili mfumo uliopo kwenye vyombo vya habari, inapaswa kuvunja ukimya kwa kuwawezesha hususan wanawake wanahabari.

Alisema ili kufikia usawa ndani ya vyumba vya habari, inatakiwa kubadili utamaduni uliopo kwa wanawake kujiendeleza na kuwa viongozi.

"Waandishi kwa muda mrefu mnatimiza  wajibu wenu wa kuwa sauti ya wasio na sauti, lakini msisahau kujisemea wenyewe kwa kuzitatua changamoto zenu," alisema Msasanuri.

Alieleza kuwajumuisha wanaume katika kufahamu changamoto zinazowakumba wanawake, kama vile za kijinsia kutatatua tatizo la rushwa ya ngono ambayo imekuwa ikitumika kwa baadhi yao kuinua mazingira ya kazi.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Tanzania (JOWUTA), Suleiman Msuya, akimkabidhi cheti mshiriki Christina Mwakangale.
Mshiriki wa mafunzo Tatu Mohamed akipokea cheti kutoka kwa Katibu wa JOWUTA, Suleiman Msuya.
 
Katibu Mkuu akiwa na washiriki wa mafunzo.

No comments:

Post a Comment

Pages