HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 13, 2019

YEV, UHC WAHIMIZA BIMA YA AFYA KWA WOTE

 Mkurugenzi wa YEV, Jonathan Kassib, akihimiza jambo alipozungumza na umma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Bima ya Afya Duniani.
 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Silas Wambura, akizungumzia mpango wa Serikali kuhusu Sheria ya Bima ya Afya kwa kila Mtanzania.
 Washiriki wa maadhimisho hayo, yaliyofanyika Bwalo la Jeshi la Akiba (Mgambo) jijini Mwanza.



Na Mwandishi Wetu, Mwanza



SHIRIKA la Youth & Environment Vision (YEV) na washirika wake, Universal Heath Coverage (UHC), wamehimiza kufikiwa haraka malengo ya Milenia, kwa kila mwananchi kuwa na bima ya afya.

Umoja wa Mataifa (UN) unataka ifikapo mwaka 2030, suala la usawa liwe limefikiwa kwa kila nchi duniani, ili kuharakisha maendeleo na ustawi wa jamii kwa ujumla.



Ushauri huo umetolewa jijini Mwanza na Mkurugenzi wa YEV, Jonathan Kassib, alipozungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Bima ya Afya kwa Wote, inayoadhimishwa Desemba 12 kila mwaka ulimwenguni kote.

"Moja ya malengo ya Milenia ni kudhibiti umasikini, vifyo vya mama na watoto, kuboresha afya na elimu.



"Tanzania ilishasaini mkataba wa wa kimataifa kuridhia masuala ya usawa, ambapo shinikizo la Dunia ifikapo mwaka 2030, mambo hayo yawe yamefikiwa," Kassib ameueleza umma.


Kwa jijini Mwanza, maadhimisho hayo yaliratibiwa na YEV kwa kushirikiana na wahisani wake Universal Heath Coverage (UHC),
TCRA-CCC, HAPSS. Kwa mujibu wa YEV, suala la kila mtu kuwa na bima ya afya ni jambo
linalopaswa kutiliwa mkazo zaidi, ili kuimarisha usawa wenye maendeleo endelevu katika jamii.



Ameupongeza uongozi wa Universal Heath Coverage kwa namna
walivyofanikisha maadhimisho hayo, pamoja na wahisani wengine na jamii
 kwa ujumla wake.

 DMO

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Silas Wambura, amesema suala la kila mtu kuwa na bima ya afya tayari limeshaanza kufanyiwa kazi na Serikali.

Amesema kwa sasa Tanzania inafanya utafiti juu ya jambo hilo muhimu katika maendeleo ya jamii, kabla Muswada wa Sheria ya kila mtu kuwa na bima haujawasilishwa bungeni. 

"Hili ni jambo zuri sana. Serikali italeta sheria baada ya utafiti
ambapo kila mtu atatakiwa kuwa na bima ya afya. "Wale wasiojiweza watahudumiwa na Serikali," amesema Dk. Wambura huku
akisema zaidi ya zahanati 400 zimepanuliwa mkoani Mwanza.



Kulingana na Mganga Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, jumla ya zahanati 105 zinajengwa mkoani hapa, huku kukiwa na mkazo zaidi wa kila kijiji kuwa na huduma za kiafya.



Amehimiza familia kuwa na bima ya afya ya CHF, inayotolewa kwa Sh 30,000 kwa mwaka na Shirika la Bima nchini (NHIF).

Miongoni mwa washiriki wa maadhimisho hayo, Christopher Gamaina, Seleman Paul, kutoka AIM Global na wengine wakiwamo watumishi wa Mungu, wamesisitiza kutiliwa mkazo bima ya afya kwa kila mtu.



Mwanasiasa maarufu nchini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, mkoani Kigoma, Zitto Kabwe, katika taarifa yake kwa umma jana, amehimiza suala hilo.

Zitto ameshauri Serikali kutoigeuza bima ya afya kuwa biashara, bali iwe huduma kwa kila Mtanzania apate, ili kukabiliana na maradhi yanayofifisha nguvukazi ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages