Mwakilishi wa FAO hapa Tanzania, Fred Kafeero (mwenye kapelo) akisikiliza maelezo kuhusu njia bora za kufanya kilimo hai kutoka kwa Meneja wa Mafunzo na Ubunifu wa Kituo cha SJS, Martin Mhando (wa kwanza kulia).
Mkuu wa Kituo cha Kilimo hai SJS Mwanga, Padri Alwyn de Souza (wa kwanza kushoto), akimkaribisha kituoni hapo Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Fred Kafeero (wa kwanza kulia) aliyefanya ziara fupi kituoni hapo.
Na Irene Mark
MWAKILISHI Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), Fred Kafeero ameahidi kushirikiana na uongozi wa Kituo cha Kujifunza Kilimo hai cha Mtakatifu Joseph (SJS) ili kueneza elimu hiyo hapa nchini.
Kituo SJS kipo kwenye Kijiji cha Kwanyange Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro chini ya uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Same kwa lengo la kuendeleza kilimo na kutoa mafunzo ya kutumia teknolojia asili rafiki wa mazingira.
Kafeero alitembelea kituo hicho jana ambapo kwa zaidi ya saa tano alizunguka shamba la kilimo hai kujionea uzalishaji na utengezaji wa mbolea ya mboji huku akishangazwa na ubunifu wa jokofu la mkaa linaloweza kuhufadhi mazao shambani Kwa muda mrefu.
"Tunategemea kushirikiana na SJS Organic ili kuona jinsi gani kazi yao hii nzuri sana inavyoweza kuwafikia wengi hapa Tanzania," alisema Kafeero.
Alisema kituo cha SJS kina uwezo wa kubadili maisha ya wakazi wa Mwanga kiafya na kiuchumi, hivyo FAO itasaidia kusambaza elimu na ubunifu huo kwenye maeneo mengine ili kuirejesha dunia katika matumizi ya vitu asili na kuepuka kemikali za viwandani zinazotajwa kuwa sababu ya maradhi yasiyoambukizwa.
"Niwapongeze kwa uamuzi na hatua bora mlizochukua mmenishangaza sikutegemea kuona mambo mazuri hivi mmekua na maono chanya kwenye kilimo hai na ufugaji wa asili.
"...Hakika hiki ni kituo bora cha mfano na kujivunia," alisema Kafeero alipozungumza na Mkuu wa Kituo cha SJS, Padre Alwyn de Souza baada ya kutembelea sehemu ya shamba hilo la ekari 50.
Akimshukuru mwakilishi huyo wa FAO, Padre Alwyn alisema shamba hilo lilianza mwaka 2017 baada ya Askofu wa Jimbo Katoliki Same, Logath Swai, kutembelea India na kuona jisi wanavyolima, kufuga na kutengeneza viatilifu na dawa za binaadamu na mifugo kwa kutumia teknolojia za vitu vya asili.
Kwa mujibu wa padre huyo, aliombwa na Askofu kuja kuanzisha shamba hilo akisaidiwa na Meneja wa Mafunzo na ubunifu mtanzania Martin Mhando na wasaidizi wengine wasiozidi 15.
"Tunasambaza upendo kwa wengine hasa wanavijiji wanaotuzunguka ili nao wajifunze kilimo hai na teknolojia asili kwa maendeleo yao na Tanzania.
"Lengo letu ni kukifanya kituo hiki kuwa Chuo maalum kwa mafunzo ya kilimo hai na ufugaji wa asili ili watu waje kujifunza kwa vitendo na kulinda afya zao na kujipatia kipato bora," alisema Padre Alwyn.
No comments:
Post a Comment