Na Irene Mark, Moshi
WAKULIMA na wadau wa kilimo hai zaidi ya 12,000 kutoka ndani
na nje ya Tanzania wanakutana kesho mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya
maonesho ya mazao mbalimbali yatokanayo na kilimo hai na kubadilishana uzoefu.
Maonesho hayo ya kila mwaka yatafanyika kwenye viwanja vya
Ushirika mjini hapa ambapo Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, atazungumza
na wakulima hao ambapo pamoja na mambo mengine watajadili changamoto za kilimo
hai na njia za kukabiliana nazo.
Mshauri wa masuala ya Kilimo Hai kutoka Shirika la
kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Constantine Akitanda, alisema wakulima
na wadau hao wa kilimo hai wanatoka nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na
Marekani.
Akitanda alizungumza hayo mbele ya waandishi wa habari zaidi
ya 25 wanaopata mafunzo ya siku mbili kuhusu kilimo hai kwa vitendo katika Kituo
cha Kilimo Hai cha Mtakatifu Joseph, kilichopo eneo la Kwanyange Mwanga mkoani
Kilimanjaro kinachosimamiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Same.
Maonesho hayo yameandaliwa na Shirika lisilo la Serikali
lenye makao yake makuu Moshi mkoani humo la (Flora & Fauna Restoration System
Tanzania) FLOFRESTA Tanzania, chini ya kaulimbiu isemayo ‘Kufikia uchumi
endelevu wa viwanda na uhakika wa chakula kupitia ubunifu wa kilimo endelevu’.
Kwa mujibu wa Akitanda, viongozi wa ngazi na sekta tofauti
za Serikali watahudhuria maonesho hayo ili kujifunza mbinu sahihi za kilimo hai
na kununua mazao yatokanayo na kilimo hicho.
Mkurugenzi wa FLOFRESTA Tanzania, Richard Mhina alisema
lengo la maonyesho hayo ni kubadilishana
uzoefu na kujifunza mbinu bora za kilimo ili kukuza kilimo cha kibiashara
katika kufikia uchumi wa viwanda na kuongeza kipato cha familia na taifa.
“Katika maonesho haya tumeshirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo
Shirika la Chakula Duniani (FAO), Swiss Aid, Ubalozi wa Ufaransa, TOAM, SAT,
NEMC, TAHA, Vyama vya kiraia, Sekta binafsi, Taasisi za utafiti, Wasomi, Viongozi
wa dini, Wanasiasa, Wafanyabiashara na ninyi waandishi wa habari.
“Maonesho haya yanatarajiwa kutengeneza na kuongeza fursa za
masoko ya bidhaa za kilimo hai miongoni mwa wakulima na walaji, ikihuisisha
masoko ya ndani na nje ya nchi… hii ni fursa kwa wasindikaji wa mazao ya mboga
na matunda kufanya biashara na kujenga miundombinu imara ya uzalishaji wa
malighafi zinazohitajika katika viwanda vidogo vya usindikaji,” alisema Mhina.
Alisema maonesho ay aina hiyo yanafanyika kwa miaka sita
mfululizo na vikundi 450 vya wakulima vyenye wanachama 11,294 hushiriki maonyesho
ya kilimo, biashara na kupata fursa ya kujifunza mbinubora za kilimo na
kusindika mazao ya mboga na matunda.
Mhina alisema FLOFRESTA Tanzania inao mpango wa kuotesha
miti ambapo chini ya mpango huo huotesha miti 1,500,000 kila mwaka na wamefanya hivyo kwa miaka 10 mfululizo.
Alisema miti hiyo huoteshwa pembezoni mwa vyanzo vya maji,
maeneo ya wazi, kando ya barabara na kwenye mashamba ya watu binafsi.
No comments:
Post a Comment