Mkurugenzi Idara
ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe na
Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto, wakisoma Jiwe la
uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa Bomba la mafuta, wakati walipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu
na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa na
kushauri mipango ya menejimenti ya maafa ya mikoa linakopita bomba
hilo izingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri mradi huo. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Ibrahim Hamidu
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, imezishauri Kamati
za Usimamizi wa Maafa katika mikoa 8 na vijiji 184
vinavyopatikana katika wilaya 24 zilizopo katika mikoa ya Kagera, Geita,
Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, ambapo Mradi wa Bomba la
Mafuta utatekelezwa kuuweka Mradi huo katika Mipango yao ya kujiandaa na
kukabiliana na Maafa ili kuhakikisha mradi huo hauthiriwi na majanga yanayoweza
kutokea.
Kwa
mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015,
inaainisha majukumu ya kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya
Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutoa
taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika, Kuratibu na kusimamia shughuli za
usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji wilaya au
mkoa, pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika
ngazi husika.
Akiongea mara baada ya kutembelea eneo la kwenye peninsula ya
Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo
utatekelezwa, Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kanali Jimmy Matamwe amefafanua kuwa Kamati za maafa zinalo jukumu la kuchukua
tahadhari ya namna ya kuhakikisha majanga yanayoweza kuuathiri mradi huo
yanakuwa katika mipango yao ya menejimenti ya maafa ili faida zitakazotokana na
utelelezaji wa mradi huo zinakuwa endelevu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa
Tanga, Noel Kazimoto ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa za
kiuchumi kwa watanzania hivyo ni dhahiri kuwa eneo la Chongoleani litakuwa na
mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zitakuwa
zikiendeshwa, kwa kuwa wananchi ni wadau wa menejimeti ya maafa kupitia kamati
za menejimenti za maafa kuanzia ngazi ya vijiji, wataendelea
kuelimishwa juu ya majanga yanayoweza kuuathiri mradi huo ili waweze
kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.
Kwa mujibu wa
Tovuti rasmi ya Kampuni inayojenga mradi huo, East African Crude Oil
Pipeline www.eacop.com. Kampuni
hiyo inabainisha kuwa wanao mpango unaohakikisha utelezaji wa mradi huo
unazingatia majanga na maafa wakati wa kupanga, kujenga na kuendesha Bomba,
ambapo Mpango huo unahakikisha kwamba, katika tukio la dharura linaloweza
kutokea, hatua za haraka, zinachukuliwa.
Mradi
wa Bomba la Mafuta Ghafi unatekelezwa kwa
ubia wa ujenzi na uendeshaji kwa kushirikisha kampuni za Total ya Ufaransa,
CNOOC ya China, Tullow ya Uingereza na Serikali za Tanzania na Uganda. Mafuta
ghafi yatasafirshwa kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi
bandari ya Tanga nchini Tanzania. Mradi wa
Bomba hilo una umbali wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 298 zitakuwa nchini
Uganda, na kilometa 1,147 zitakuwa nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment