Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo
kuhusiana na Mradi wa Nyumba za Shirika la Nyumba za Taifa (NHC) uliopo eneo la
Ilembo Manispaa ya Mpanda mkoa wa Katavi kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa
Shirika hilo Muungano Saguya jana wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya NHC
mkoani Katavi. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga na
kushoto ni Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Katavi na Rukwa Msumbuko Majaliwa. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM KATAVI
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelipongeza Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Katavi kwa kuwa moja ya mkoa wenye miradi mingi
ya Shirika hilo.
Dkt Mabula alitoa pongezi
hizo jana wakati akikagua miradi ya NHC kwenye mkoa wa Katavi akiwa katika
ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na ujenzi wa
miradi inayotekelezwa na Shirika la
Nyumba la Taifa.
Miradi aliyoikagua Naibu
Waziri Mabula katika mkoa wa Katavi ni ujenzi wa nyumba za watumishi katika
Halmashauri ya wilaya ya Mlele, Ofisi na Nyumba ya Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) pamoja na ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda. Pia
alikagua mradi wa nyumba sabini za Ilembo ambapo Nyumba kumi kati ya hizo
ziliuzwa na nyumba sitini zimepangishwa.
Alisema, mkoa wa Katavi
unaweza kuwa mkoa wa kwanza ama wa pili kwa kuwa na miradi mingi ya Shirika la
Nyumba la Taifa na hali hiyo siyo tu inaonesha jinsi Shirika lilivyo makini kwenye
uwekezaji miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa nyumba za kuuza, kupangisha na majengo
ya biashara bali inalifanya kuimarika kimkoa.
Akigeukia mradi wa Jengo
la Biashara la Paradise lililopo Manispaa ya Mpanda, Dkt Mabula alilisifu jengo
hilo kwa kuwa na mazingira mazuri ya kibiashara na kushauri taasisi za serikali
katika mkoa wa Katavi kutumia fursa ya kupanga na kuwekeza kwenye jengo hilo
kwa kuwa gharama zake ni nafuu ukilinganisha wapangishaji wengine.
Aidha, amelitaka Shirika
la NHC mkoa wa Katavi kuhakikisha inalifanyia matangazo jengo hilo la biashara
la Paradise kwa lengo la kuvutia wateja kupanga hasa ikizingatiwa kutolitangaza
kunaweza kusababisha kukosa wateja.
Kauli hiyo ya kutaka
kufanyika matangazo kwenye jengo hilo inafuatia Naibu Waziri Mabula kuelezwa na
Kaimu Meneja wa Shirika la NHC mkoa wa
Katavi na Rukwa Masumbuko Majaliwa kuwa mpaka sasa jengo hilo la kibiashara
limepangisha asilimia thelathini tu ya wateja.
‘’Mrudi kwenye kutangaza
miradi yenu kupitia kipindi cha Maisha ni Nyumba na ikiwezekana kazi hiyo ifanyike
mkoa kwa mkoa na mhakikishe miradi yenu mnaifanya kwa kasi, viwango na wakati ili
kujenga trust kwa wateja’’ Alisema Dkt Mabula.
Kwa upande wake Meneja
Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya alisema, kwa sasa Shirika lake linafanya
vizuri katika masuala ya ujenzi jambo lililosababisha kuaminwa na serikali
ambapo katika mji wa serikali eneo la Mtumba Dodoma liliweza kujenga majengo ya
Wizara nne na sasa Shirika linaendelea na utekelezaji wa miradi mingine kama
vile ujenzi wa nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
nchi nzima.
Awali Kaimu Meneja wa
Shirika la Nyumba mkoa wa Katavi na Rukwa Masumbuko Majaliwa alimueleza Naibu
Waziri kuwa kwa sasa NHC mkoa wa Katavi inatekeleza miradi mbalimbali katika
mikoa ya Katavi na Rukwa.
Alisema katika mkoa wa
Katavi Shirika la Nyumba linatekeleza miradi ya nyumba za watumishi Mlele,
ukumbi wa manispaa ya Mpanda pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu Kibaoni
wakati upande wa mkoa wa Rukwa miradi inayotekelezwa ni ile ya mradi wa nyumba
za makazi jangwani Sumbawanga pamoja na duka la dawa katika hopspitali ya rufaa
mkoa wa Rukwa.
No comments:
Post a Comment