Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu
maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum,
Zainab Katimba kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Januari 30,
2020
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) kwenye viwanja vya Bunge jijini
Dodoma, Januari 30, 2020. Kulia ni Mbunge wa Baraza la
Wawakilishi, Jaku Ayoub.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema licha ya kuwepo kwa ugatuaji wa madaraka (D by D), Serikali
za Mitaa bado zina wajibu wa kuwahudumia wananchi kwa sababu ziko karibu nao zaidi
kuliko Serikali Kuu.
Ametoa kauli
hiyo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati akijibu
swali la mbunge wa Viti Maalum, Bi. Ruth Mollel, kwenye kipindi cha maswali kwa
Waziri Mkuu bungeni. Mbunge huyo alisema dhana ya ugatuaji wa madaraka inakinzana
na hali halisi kwani utekelezaji wake haujaenda sawasawa kwa vile Serikali
inakusanya fedha kutoka kwenye vyanzo vya mapato vya Halmashauri kama vile kodi
ya majengo na mabango.
“Wajibu wa
kumhudumia mwananchi ni wa Serikali za Mitaa kwa sababu iko karibu nao zaidi.
Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kuwa tunashirikiana na Serikali za Mitaa
kumhudumia mwananchi lakini hatujaondoa wajibu wa Serikali za Mitaa kuwahudumia
wananchi,” amesisitiza.
Amesema Serikali Kuu bado inalo jukumu la kusimamia
mapato na imeamua kudhibiti ukusanyaji wa mapato na imekuwa ikihakikisha mapato
haya yarudi tena kwa wananchi. “Tunaporudisha kwa wananchi, tunawapelekea hao
hao Serikali ya Mitaa kwa mahitaji yao ili watekeleze hilo jambo,
hatujawaondolea mamlaka ya kusema tunahitaji darasa, tunahitaji kituo cha afya,
tunahitaji uboreshaji wa miundombinu.”
“Tumeongeza hata taasisi kwa kuunda TARURA ili isimamie miundombinu; sasa
hivi tunaenda kwenye maji, kutakuwa na taasisi ya kusimamia utoaji wa maji.
Pale ambapo kuna mahitaji, Mamlaka ya Serikali za Mitaa iseme inahitaji
shilingi ngapi, kwa ajili ya nini, nasi tunawapelekea, ndiyo kwa sababu leo
tunaona huduma zinatekelezwa mpaka vijijini. Hii ni kwa sababu tunashirikiana
na Serikali za Mitaa katika kuratibu.”
“Ule udhaifu
wa usimamizi wa makusanyo, na udhaifu wa usimamizi wa matumizi ambao ulikuwa
umejitokeza sasa tunaendelea kuutibu na ndiyo kwa sababu unaona wakati wote
tunapokwenda huko kwenye ziara, kwanza tunauliza ukusanyaji na kama makusanyo
yoyote yamehifadhiwa na matumizi yake yako sawa, na pale ambapo matumizi
yanakuwa si sahihi tunachukua hatua,” amesema.
Amesema
kutokana na muundo uliopo, zipo Serikali za Mitaa ambazo zina majukumu yake
yaliyoainishwa rasmi na kuna Serikali Kuu ambayo pia inawajibika kuzihudumia Serikali
za Mitaa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema haitaleta maana
endapo Serikali italazimika kutengua matokeo ya uchaguzi wote wa Serikali za
Mitaa wakati wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo hayo walikuwa na fursa
ya kukata rufaa.
“Chaguzi zote
nchini zinatawaliwa na kanuni na sheria zake. Kila mmoja aliyeshiriki kama
aliona kuna ukiukwaji wowote, alikuwa na fursa ya kukata rufaa na kama
hajaridhika, alikuwa na fursa ya kwenda mahakamani,” alisema.
Alisema chaguzi
zote zina sheria zake na kanuni zake na hata wakati wa kuandaa kanuni za
Serikali za Mitaa, vyama vyote vya siasa vilishirikishwa katika kutengeneza
kanuni zao na moja kati ya kanuni hizo ni pale ambapo inatoa fursa kwa yeyote ambaye
hajaridhika huko anakogombea, anaweza kukata rufaa na atakapoona rufaa hiyo
kwenye ngazi inayofuata haikutenda haki, aende mahakamani.
“Kwa hiyo
kulichukua hili kwa ujumla ujumla, inaweza isiwe sahihi sana kwa sababu kila
mmoja kule alipo, alikuwa na mamlaka yake inayoratibu na anayo fursa ya kwenda
kwenye mamlaka kukatia rufaa pale ambapo hajaridhika na utekelezaji wa jambo hilo.
Na vyama vyote vilishiriki kwenye hii kanuni ya kukata rufaa, kwa hiyo ni
wajibu wa huyo mgombea kwenye eneo hilo kwenda kukata rufaa,” alisema.
Alikuwa akijibu
swali la mbunge wa Mbozi, Bw. Pascal Haonga, aliyetaka kujua kama Serikali iko
tayari kurudia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba,
mwaka huu kwa sababu ule uliopita uligubikwa na dosari nyingi.
“Mchakato wa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa mwaka 2019, uligubikwa na dosari nyingi sana zikiwemo za wagombea kutoka
vyama vya upinzani kunyimwa fomu, ofisi kufungwa kwa muda wote, hivyo kupelekea
baadhi ya wagombea hasa wa upinzani kushindwa kupata fursa za kugombea. Serikali
haioni kwamba ni vema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uweze kurudiwa sambamba na uchaguzi
mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu?” alihoji.
No comments:
Post a Comment