Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb) akijibu
maswali ya Wabunge wakati wa Bunge la Kumi na Nane Jijini Dodoma hii leo tarehe
7 Februari, 2020.
NA MWANDISHI WETU
Serikali imetenga takribani ekari
laki mbili katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni mikakati wa kukuza na
kuendeleza shughuli za maendeleo ya vijana.
Hayo yamesemwa na Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.
Anthony Mavunde (Mb) Februari 7, 2020 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Grace Tendega aliyetaka kufahamu juu ya utekelezaji
wa Serikali katika kuendeleza shughuli za vijana.
Naibu Waziri Mavunde alieleza
kuwa Serikali imetenga maeneo ya shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la
kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na itakayo
wanufaisha kiuchumi.
“Serikali itaendelea kuzihamasisha
Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za Vijana ikiwemo
kilimo, viwanda na ufugaji ili kuwapa vijana fursa ya kuyatumia maeneo hayo katika
shughuli zitakazowaletea maendeleo,” alisema Mavunde.
Wakati huo huo, Mhe. Mavunde alitoa
ufafanuzi kwa Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Simon Msigwa (Mb) ambaye aliuliza kuhusu
Mpango wa Serikali katika kutoa mafunzo kwa vijana ambao wamehitimu ili waweze kukidhi
soko la ajira?
Alieleza kuwa Serikali
Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi nchini
ambayo inalenga kuimarisha nguvukazi inapata ujuzi unaotakiwa katika soko la
ajira.
Akifafanua baadhi ya Programu
ambazo zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na Mafunzo ya Kurasimisha Ujuzi
uliopatikana nje ya Mfumo usio rasmi, Mafunzo ya Uanagenzi ambayo yanatolewa kwa
njia ya ufundi wa fani mbalimbali na Mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa Teknolojia
ya Kitalu Nyumba “Greenhouse”, Mafunzo ya Vitendo Mahali pa Kazi kwa wahitimu
n.k.
Aidha alielezea suala la ukosefu
wa ajira kwa vijana waliohitimu katika elimu ya juu kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu,
“Jitihada za Serikali imekuwa ikiwapeleka vijana hao katika makampuni na
viwanda mbalimbali ambapo wanapata mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi 6 hadi
12 na baada ya hapo wanapatiwa cheti cha
Utambuzi “Certificate of Recognition”, cheti hiko kinawasaidia vijana hao kuwa wanauzoefu
wa kazi Fulani,” alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa Serikali
imekuwa ikiwafadhili vijana kwa kuwapatia mafunzo ya Ufundi stadi katika Vyuo
vya Veta, Don Bosco na Vyuo shirikishi ili kuwawezesha vijana wanapata ujuzi unaostahili
katika soko la ajira.
No comments:
Post a Comment