*Maboresho yagusa vyuo
vya ualimu, VETA na ujenzi wa mabweni
*Wanafunzi 130,072 wa elimu ya juu waata mikopo ya sh. bilioni 266.4
SERIKALI
imetoa jumla ya shilingi bilioni 128.1 kwa ajili ya kugharamia elimumsingi
bila ada katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2019.
Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa leo (Ijumaa,
Februari 7, 2020) wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 18
wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi
31, mwaka huu.
“Serikali imeboresha elimu ya msingi
kwa kuendelea kutekeleza programu ya elimumsingi bila ada ambapo Serikali
inagharamia chakula kwa wanafunzi 189,226 wa kutwa na bweni, posho ya madaraka
kwa walimu wakuu 23,843, fidia ya ada kwa wanafunzi 1,874,331 na ruzuku ya
uendeshaji wa shule,” amesema.
Akielezea
kuhusu matokeo ya mitihani ya kitaifa, Waziri Mkuu amesema matokeo chanya ya
maboresho hayo ni kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika upimaji wa kitaifa
kwa darasa la nne, kidato cha pili na mitihani ya kitaifa kidato cha nne kwa
kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019. “Shule za Kata nazo zimeendelea
kufanya vizuri na kuongeza matumaini kwa Watanzania walio wengi,” ameongeza.
“Matokeo
ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kwa mwaka 2019, yamebainisha kuwa jumla
ya wanafunzi 1,531,120 walifaulu ikilinganishwa na wanafunzi 1,213,132
waliofaulu mwaka 2018. Ufaulu huo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.21. Kwa upande
wa kidato cha pili, wanafunzi 514,251 walifaulu upimaji wa kitaifa kwa mwaka
2019 ikilinganishwa na wanafunzi 452,273 waliofaulu upimaji huo mwaka 2018 sawa
na ongezeko la asilimia 13.7,” amesema.
“Kwa
upande wa kidato cha nne, mwaka 2019 wanafunzi 340,914 kati ya wanafunzi
422,722 walifaulu mtihani wa taifa wa kidato cha nne. Ubora wa ufaulu wa wanafunzi
nao umeongezeka kwa mwaka 2019. Kwa mfano, wanafunzi 135,301 sawa na asilimia
32.01 walipata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu,” ameongeza.
Akielezea
kuhusu maboresho ya miundombinu ya eimu, Waziri Mkuu amesema maboresho na
uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu yamekuwa chachu ya kuongezeka kwa kiwango
cha ufaulu na wakati mwingine kuleta changamoto kwenye miundombinu ya elimu.
“Hata
hivyo, Serikali imeendelea kukamilisha usajili wa shule mpya, kuongeza vyumba
vya madarasa 1,218 na mabweni 14 ili wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato
cha kwanza mwaka 2020, waweze kuanza masomo kwa wakati,” amesisitiza.
Akitoa ufafanuzi kuhusu maboresho
kwenye elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeimarisha elimu ya juu, ufundi na ustawi wa jamii kwa
kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo hadi Desemba mwaka
jana, sh. bilioni 266.4 zimetolewa kwa wanafunzi 130,072. “Kati yao, wanafunzi
49,493 ni wa mwaka wa kwanza na 80,579 wanaoendelea,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kujenga
mabweni ya wanafunzi wa kike; kukarabati majengo ya vyuo vikuu na vyuo vya
ualimu; kuboresha vyuo vya VETA kwa kujenga na kuboresha vyuo na kununua vifaa
vya kufundishia na kujifunzia.
“Vilevile, Serikali imeimarisha vyuo
vya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwa kuanzisha vituo vya ubunifu
vitano sambamba na kutekeleza programu ya uanagenzi ili wapate ujuzi wa
kujiajiri unaoendana na ushindani wa soko la ajira,” amesema.
No comments:
Post a Comment