Na Christina Mwakangale
WAKATI ya virusi vya
Corona (COVID-19) vikizidi kushika kasi katika nchi tofauti tofauti, Tanzania
imesitisha safari za nje ya nchi zisizo za lazima kwa watumishi wa umma.
Rais John Magufuli
ameagiza ianze kampeni ya kuuelimisha umma juu ya virusi vya Corona katika
mikusanyiko ya watu.
Rais Magufuli alitoa
agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Karakana Kuu ya Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), Lugalo.
Alisema Tanzania bado
haina taarifa ya mgonjwa mwenye maambukizi hayo na ameagiza elimu iendelee
kutolewa katika maeneo yote ikiwamo vyuoni na shuleni.
Virusi vya Corona
ambavyo vimeenea kwa nchi zaidi ya nchi 14 za Asia, Ulaya na Afrika, vilianzia
mji wa Wuhan jimbo la Hubei, nchini China, Desemba mwaka jana.
Takwimu za hadi Machi
13 mwaka huu, zinaeleza kuwa kuna taarifa za watu 136,597 na jumla ya watu
5,065 wamekwishafariki dunia kutokana na virusi hivyo, huku idadi kubwa ya vifo
ikiwa China ambako tayari kuna vifo 3,179 ikifuatiwa na Italia 1,016.
Licha ya virusi vya
Corona kutishia mataifa mbalimbali ambayo baadhi yameamua kusitisha safari za
ndege, kuzuia mikusanyiko ya watu na kufunga mipaka yao, Rais Magufuli
amewataka Watanzania wachukue tahadhari.
“Virusi vya Corona vipo
duniani na vimeikumba nchi nyingi duniani na virusi vinasambaa kote lakini
Tanzania hadi sasa hatujapata mgonjwa, hatuwezi kujiweka pembeni ni vizuri
kuendelea kuchukua hatua na tahadhari,” alisema Rais Magufuli na kuongeza…
Lazima tujikinge, kama
safari si ya lazima usisafiri, hatutatoa vibali kusafiri bila sababu hata
Watanzania kusafiri kuwe na sababu.”
Pia rais alisema kuwa
tahadhari itolewe kwa watu wote na si kuachiwa viongozi pekee na kwamba
amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kutoa vibali vya safari kwa
watumishi, iwapo kuna ulazima.
“Kampeni ifanyike
katika kuelezea ugonjwa huu katika daladala, vyombo vya habari vitoe habari,
mkilisimamia hili mtashinda, wanahabari hili ni jukumu lenu. Pia tuepushe
mikusanyiko wakuu wa mikoa, wilaya, serikali, wote,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alisema kuwa kutokana
na virusi hivyo ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), ambayo imefanya
safari yake jana kuelekea nchini India, haitafanya tena safari kuelekea nchini
humo.
“ATCL iliyokwenda India
ikirudi leo, haitaenda tena, tumuombe Mungu kila mmoja katika imani yake, sasa
nchi inakwenda vizuri kiuchumi ugonjwa huu ukiingia unaweza kurudisha nyuma
tulipo,” alisema Rais Magufuli.
Wakati habari za Virusi
vya Corona zikiendelea kutawala vichwa vya habari vya mitandao ya kijamii na
vyombo vya Habari, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imekana kuwa haijatenga Hospitali ya Mloganzila kuwa karantini ya wagonjwa
watakaobainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo.
Hata hivyo jana taarifa
zilizotolewa na moja ya hospitali kubwa (jina tunalihifadhi) jijini Dar es
Salaam, ilitangaza kubaini mgonjwa mmoja wa Corona ambaye ni raia wa India.
Taarifa ya hospitali
hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa alifika hospitalini hapo Machi 12 mchana, akiwa
na dalili za ugonjwa huo ambapo walimuweka sehemu maalum kumchunguza zaidi.
Ilibainisha kuwa baada
ya kufanya hivyo waliitarafu serikali juu ya uwepo wa mgonjwa huyo.
Hata hivyo taarifa hizo
zilikanushwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Gerald Chami, alipozungumza na
TanzaniaDaima juu ya uvumi huo.
“Taarifa zilizosambaa
mtandaoni si za kweli hatuna mgonjwa wa Corona hadi sasa hapa Tanzania wala
hospitali ya Mloganzila haijatengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Corona” alisema.
Mkenya akutwa na Corona
Wakati Tanzania ikisema
haina mgonjwa wa Corona, Kenya imethibitisha kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza mwenye
virusi hivyo.
Waziri wa Afya wa
Kenya, Mutahi Kagwe alisema mtu mwenye maambikizi ya virusi vya Corona alibainika
juzi usiku.
Alibainisha kuwa Mkenya
huyo aliwasili nchini humo kutoka Marekani kupitia jijini London, Uingereza
tangu Machi 5, mwaka huu.
Aligundulika kuwa na
virusi hivyo katika maabara ya wizara ya Afya nchini Kenya.
Hata hivyo waziri huyo
alisema, mgonjwa huyo ambaye ni mwanamke yuko katika hali njema na viwango
vyake vya joto vimeshuka na kuwa vya kawaida.
Katika hatua nyingine Waziri
huyo amewataka Wakenya kuwa watulivu na kuacha wasiwasi kwa kuwa serikali yao inaendelea
kuimarisha mikakati ili kuhakikisha virusi vya Corona havisambai zaidi.
Waziri Kagwe aliwataka
Wakenya kunawa mikono mara kwa mara, kutokaribiana zaidi na mtu mwingine anayekohoa
ama kupiga chafya, watu wanaokohoa ama kupiga chafya wasalie majumbani mwao ama
kutojichanganya na makundi ya watu.
Mengine ni watu kuziba pua
na mdomo wanapokohoa kwa kutumia kitambaa ama tishu, . Mtu anayehisi joto ama
tatizo la kupumua ametakiwa kusalia nyumbani.
Pia serikali ya Kenya
imepiga marufuku mikutano ya aina yote ikiwemo ile ya umma ikiwemo ya kidini,
michezo huku ikiwataka wanaotaka kwenda makanisani na misikitini kunawa mikono
na sabuni kabla ya kuingia katika sehemu hizo.
Kenya pia imezuia michezo
yote inayohusisha shule, wachukuzi wa umma na abiria kunawa mikono yao kabla ya
kuingia katika magari hayo.
Pia Wakenya wamezuiwa kutoka
nje ya nchi isipokuwa wale wenye umuhimu mkubwa wa kusafiri na hakuna mtu atakayeruhusiwa
kuelekea katika mataifa yenye visa vingi vya ugonjwa huo.
DRC nako si shwari
Nako Jamhuri ya Kidemorasia
ya Congo (DRC) kimeripotiwa kisa cha pili cha maambukizi ya virusi vya ugonjwa
wa Corona.
Mwandishi wa Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC) mjini Kinshasa, mtu huyo anadaiwa ni raia wa
Cameroon aliyewasili nchini humo kutoka Ufaransa.
Kwa sasa amelazwa
hospitalini kwa matibabu huku Wizara ya Afya nchini humo ikitoa wito kwa raia
kuzingatia usafi wakati wowote.
Mgonjwa huyo ni raia mwenye
umri wa miaka 46 ambaye anaishi DR Congo na familia yake.
Alirudi nchini humo
kutoka Ufaransa Mei 8, mwaka jana na
hakuonyesha dalili za virusi hivyo.
Mamlaka ya DR Congo
inasema, kufikia sasa imewatambua watu 117 waliogusana na wagonjwa wawili wa
virusi hivyo.
Taarifa hizo zinatokea
siku moja baada ya madaktari nchini DR Congo kuamua kurudi kazini wakisitisha
mgomo wa miezi miwili.
Ujerumani
wachukua hatua
Maofisa mjini Berlin, nchini
Ujerumani wametangaza kuwa mji huo utaanza kuzifunga hatua kwa hatua shule
zote, chekechekea na vituo vya kulea watoto kuanzia wiki ijayo, huku usafiri wa
umma ukipunguza ratiba zake.
Kituo cha televisheni cha N-Tv
nchini Ujerumani kimetangaza taarifa hiyo baada ya kumnukuu Meya wa Berlin,
Michael Mueller kuwa sekondari zitaanza kufungwa Jumatatu ijayo.
Wito umekuwa ukiongezeka nchini
Ujerumani kuchukua hatua sawa na zile zilizochukuliwa na nchi jirani za Ulaya,
kuzifunga shule kusaidia kupunguza kuenea kwa virusi vya Corona.
Lakini, kutokana na mfumo wa
ugatuzi, ni serikali za majimbo pekee ndiyo zenye mamlaka ya kutoa matamko kama
hayo.
Majimbo ya Saarland na Bavaria
yametangaza kuzifunga shule zote kuanzia Jumatatu ijayo.
Jimbo la Bavaria kwa upande wake,
linazifunga shule zote, chekechea na vituo vya kulea watoto hadi mwishoni mwa
likizo ya sikukuu ya Pasaka, katikati ya Aprili ili kukabiliana na janga
la virusi vya Corona.
Kwa upande wake jimbo la Saarland
limesema litazifunga shule zote katika kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo
vya COVID-19.
Waziri Mkuu wa Saarland, Tobias
Hans alisema kufungwa shule hizo ni hatua ya tahadhari kutokana na jimbo hilo
kupakana na mkoa wa Grand Est ulioko Kaskazini Mashariki mwa Ufaransa.
Majimbo mengine matatu ya
Ujerumani likiwemo la North Rhine Westphalia leo yanatarajia kuamua kuhusu
kuzifunga shule zake.
Hayo yanajiri wakati ambapo Ijumaa,
Ujerumani imetangaza kifo cha sita kutokana na virusi vya Corona, huku watu
2,000 wakiwa wameambukizwa nchini humo.
Ufaransa
Ufaransa nayo imesema itazifunga
shule zote za msingi na sekondari pamoja na chekechea kuanzia Jumatatu ijayo.
Ubelgiji na Ureno nazo
zimetangaza kuzifunga shule zake, huku shule na vyuo vikuu nchini Italia
zikiendelea kufungwa nchi nzima kutokana na taifa hilo kuathirika zaidi na
virusi vya Corona.
Nchi 15 Afrika shida
Aidha, nchi za Kenya, Ghana na
Gabon zimetangaza visa vya kwanza vya Corona, hivyo kuifanya idadi jumla ya
nchi zilizothibitisha kuhusu virusi hivyo barani Afrika kufikia 15.
Msemaji wa Shirika la Afya
Duniani, WHO, Tarik Jasarevic amezitolea wito nchi zote duniani kushirikiana
katika juhudi za kutafuta suluhisho la virusi vya Corona ambavyo vimetangazwa
kuwa.
Mke wa Waziri Mkuu Canada
Sophie Grégoire Trudeau, mkewe
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amepatikana na virusi vya ugonjwa hatari
wa Covid-19, baada ya kufanyiwa vipimo.
Sophie ataendelea kusalia katika
karantini kwa muda usiojulikana, ofisi ya Waziri Mkuu, Justin Trudeau imeeleza
katika taarifa yake ya juzi jioni.
"Waziri Mkuu yuko katika
afya njema na hana dalili zozote za maambukizi.
Hata hivyo, kwa tahadhari na
kulingana na ushauri wa madaktari, atawekwa karantini kwa muda wa siku 14,
"kimebaini chanzo hicho na kuongeza kuwa mkewe anaendelea,"
vizuri".
Justin Trudeau, 48, "kwa
hivi sasa" hatafanyiwa vipimo na "ataendelea na majukumu yake kama
Waziri Mkuu," ilisema ofisi yake na kuongeza kuwa Waziri Mkuu atalihutubia
taifa leo Ijumaa.
Katika ujumbe kwa raia wa Canada,
mkewe Justin Trudeau amewahakikishi raia kuwa anaendelea vizuri.
Ofisi ya Waziri Mkuu imetangaza
mapema asubuhi kwamba alifanyiwa vipimo vya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 kwa
sababu alikuwa na dalili za homa tangu kurudi kutoka London. Chanzo TanzaniaDaima
No comments:
Post a Comment