SERIKALIimeagiza
vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu vifungwe kwa muda wa
siku 30 kuanzia leo Machi 18, 2020 ili kuondoa msongamano katika maeneo
hayo na kuweza kujikinga na virusi vya corona.
Amesema
hadi leo, nchini kuna jumla ya watu watatu waliobainika kuwa na virusi
vya corona ikiwa ni ongezeko la wagonjwa wawili, mmoja ni raia wa
Ujerumani (24) aliyegundulika Zanzibar na mwingine ni raia wa Marekani
(61) aliyegundulika Dar es Salaam. Wote wapo katika uangalizi.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Machi 18, 2020) wakati
akizungumza na waandishi wa habari kwenye makazi ya Waziri Mkuu,
Oysterbay, jijini Dar es Salam.
Waziri
Mkuu amesema kwa sasa wanafunzi wengi wa vyuo wamefunga, hivyo
amewataka wasirudi vyuoni hadi watakapotaarifiwa na walioko vyuoni
wametakiwa warejee majumbani kwao ili kuondoa msongamano kwenye maeneo
hayo.
“Vyuo
vya ualimu wanafunzi wake walitakiwa kufanya mitihani mwezi Mei, Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia atafanya taratibu za
kurekebisha ratiba ya mitihani kulingana na matokeo ya hali ya
maambukizi.”
Waziri
Mkuu amewasisitiza wananchi waendelee na shughuli zao kwa umakini na
wasiwe na taharuki kwani Serikali inaendelea kulifanyia tathmini suala
hilo na kwamba itakuwa inatoa taarifa kadiri inavyohitajika.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema huduma katika maduka, masoko na za usafiri
ziendelee kutolewa kama kawaida ila kwa umakini mkubwa na kwenye vyombo
vya usafiri wa umma wahusika wahakikishe hawajazi sana abiria.
Jana,
Machi 17, 20202 Serikali ilitanga kuzifunga shule zote za awali, msingi
na sekondari kwa muda wa siku 30 na kwamba wanafuzi wa kidato cha sita
waliopaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020 nao watapaswa kusibiri Wizara
ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.
Waziri
Mkuu alisema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima
imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya
muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na
shughuli nyingine za kijamii.
Alizitaka
wizara na taasisi zizitishe semina, warsha, makongamano na mikutano
yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki toka nchi zenye maambukizi
makubwa. “Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye
maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” alisisitiza.
Akielezea
hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali ili kudhibiti ugonjwa huo,
Waziri Mkuu alisema: “Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya
makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la
Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyngine. Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iziandikie taasisi zake.”
Pia
aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe maeneo yote
yaliyobainishwa na kutengwa (vituo vya huduma na ufuatiliaji) kwa ajili
ya kuwahudumia wagonjwa endapo watajitokeza katika maeneo yao yanakuwa
na mahitaji yote muhimu na yanahudumiwa ipasavyo.
Alisema
Watanzania hawana budi kuzingatia ushauri unaotolewa na Serikali na
kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Watanzania tuache mzaha wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya
upotoshaji wa tahadhari katika jambo hili,” alionya.
Kuhusu
viongozi wa dini, Waziri Mkuu aliwaomba waendelee kushirikiana na
Serikali katika kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari za
ugonjwa huu. Pia amevitaka vyombo
vyote vya habari vishirikiane na Serikali katika utoaji wa elimu kwa
umma kuhusu kujikinga na Corona bila kufanya upotoshaji wala kuipa jamii
hofu.
Aliwataka wananchi watoe taarifa kuhusu uwepo wa mgonjwa au kupata ufafanuzi kuhusu ugonjwa huu kupitia namba za bure za 0800110124, 0800110125 na 0800110037.
No comments:
Post a Comment