HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 05, 2020

MAJALIWA: TUMESITISHA UCHIMAJI MADINI MAGAMBA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua eneo la machimbo ya madini ya Boxite   la Magamba wilayani Lushoto, Machi 5, 2020.  Wa pili kulia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, wanne kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Martine Shigela.  Aliagiza kusitishwa kwa shughuli za uchambaji katika machimbo hayo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



Na Mwandishi Maalum

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imesitisha uchumbaji wa madini ya boxite katika mlima wa Magamba wilayani Lushoto baada ya wananchi kuulalamikia mradi huo unasababisha uharibifu wa mazingira.
Hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Serikali wahakikishe wanaimarisha ulinzi katika eneo hilo mtu yeyote asiendeshe shughuli za uchumbaji wa madini hata Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) nao wasichimbe eneo hilo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo(Alhamisi, Machi 5, 2020) baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mabughai kata ya Magamba wilayani Lushoto, Tanga.
Amesema alipokea taarifa kwamba yapo malalamiko kuhusu shughuli za uchimbaji wa madini zinazoendelea kwenye mgodi huo kutoka kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa pamoja na mbunge wa Lushoto, Shabn Shekilindi. 
“Hatuwezi kuendelea na shughuli za uchumbaji wa madini kwenye eneo hili wakati wananchi wanalalamikia uharibifu wa mazingira unaosababisha na shughuli hii. Serikali yenu ni sikivu hivyo nawaomba muendelee kuiamini na kushirikiana nayo.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameagiza watu wote waliopewa leseni za kuchimba madini katika eneo hilo wazirudishe Serikalini na amemuelekeza Waziri wa Madini, Doto Biteko asimamie zoezi hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Lushoto amesema wananchi hawataki shughuli za uchimbaji wa madini ya boxite ziendelee kufanyika kwenye mlima Magamba kwa ajili ya kuzuia uharibifu wa mazingira.
Amesema katika mlima huo ndiko kwenye chanzo cha maji kinachotegemewa na wananchi pia mlima huo umezungukwa na miundombinu mbalimbali ya shughuli za kijamii, hivyo kuendelea kwa uchimbaji wa madini kutasababisha athari kubwa ikiwemo ukosefu wa maji.
Awali,Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema eneo hilo la Magamba lina leseni 22 za uchimbani lakini kutokana na mvutano wa wenye leseni na wananchi, wizara iliamua kusitisha shughuli za uchimbaji hadi watakapokubaliana.
Baada ya kuzungumza na wananchi, Waziri Mkuu alimtembelea Bi Miriam Shemndolwa ambaye ni mlemavu mkazi wa Mombo aliyemfahamu kupitia TBC alipohojiwa na Mtangazaji wa Kipindi cha Wape Nafasi, Tuma Dandi.
Apohojiwa katika kipindi hicho Bi Miriam aliomba msaada kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi ambapo alimtaja Waziri Mkuu. 
Waziri Mkuu ametoa msaada wa sh. milioni tano ili pamoja na michango mingine zimuwezesha kujenga nyumba ya kuishi yeye na bibi yake Eonica Hiza ambaye ndiye anayemlea. Kwa sasa Miriam na mlezi wake wanaishi kwenye nyumba ya mjomba wake.

No comments:

Post a Comment

Pages