HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 12, 2020

MAJALIWA: WANAVYUO CHINA WAENDELEA NA MASOMO KWA NJIA YA MTANDAO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mizengo Peter Pinda, wakati akiwasili kwenye mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi Machi 12, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifurahia jambo na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mizengo Peter Pinda, wakati akiwasili kwenye mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

  Baadhi ya wahitimu wakisubiria kutunukiwa shahada kwenye mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), yaliyofanyika katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi Machi 12, 2020. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wahitimu, kwenye mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), yaliyofanyika katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi Machi 12, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
PMO_5464 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiteta jambo na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mizengo Peter Pinda, wakati akiwasili kwenye mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU Kassim Mjaliwa amesema wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kutokana na mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona wote wanaendelea na masomo yao kwa njia ya mtandao.

“Tehama sasa imefikia katika hatua nzuri kwa sababu Mhadhili mmoja anaweza kuwafundisha wanafunzi wake wote popote walipo kwa njia ya mtandao. Tehama imewezesha wanafunzi waliozuiwa kurudi nchini China kuendelea na masomo wakiwa nyumbani kwao.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 12, 2020) katika mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi. Amesema baada ya virusi vya corona kuikumba China vyuo vilifungwa na sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasomo kwa njia ya mtandao.

Pia, Waziri Mkuu amewaeleza wahitimu wa CKHT kuwa vyeti walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe wanaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi itakayoakisi viwango vilivyoainishwa kwenye vyeti vyao. 

“Nendeni mkaidhihirishe tuzo hii ya pili katika utendaji wenu na maisha yenu ya kila siku, iwe ni katika sekta rasmi au sekta isiyokuwa rasmi.  Hakikisheni mnaonesha tofauti katika kutafuta majibu ya maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania kuhusu mustakabali mzima wa kujiletea maendeleo.”

Waziri Mkuu amesema amefuatilia kwa karibu maelezo ya Viongozi waliotangulia kuhusu umuhimu na hata mafanikio ya chuo hicho ambapo amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu sana kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

Amesema licha yachangamoto mbalimbali zilizopo, Serikali imeweza kuanzisha chuo hiko na kukiona kikiendelea kutanuka hadi nje ya mipaka ya nchi yetu.  “Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia. Tunawashukuru waasisi wa Taifa letu kwa maono haya makubwa kuhusu Tanzania.”  

Waziri Mkuu amesema Mwasisi wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliona mbali sana wakati akianzisha mchakato wa kuanzisha Chuo hiki kwa kusema angependa kuona taasisi inawawezesha watu wazima wengi waweze kuendelea na elimu ya juu pasipo kuacha kazi zao. 

Vilevile, aliongeza kwa kusema, “Kwa nchi maskini kama Tanzania, hakuna Taasisi nyingine ya elimu ya juu inayoweza kuwa ya msaada zaidi kwa watu wetu”. 

Waziri Mkuu amesema ukweli wa kauli hiyo unaendelea kudhihirishwa siku hadi siku kupitia mafanikio ya chuo hicho. “Tutake tusitake, elimu ya juu inayoweza kusaidia watanzania wengi zaidi ni hii ya kupitia mfumo wa Elimu Masafa na Huria.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa umuhimu na thamani ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na vyuo vingine utakuwa na maana tu pale ambapo vitakuwa na mchango kwenye maendeleo ya nchi. 

“Kwa miaka nenda rudi, chuo kimehitimisha wataalamu lukuki, ambao wengi wameingia kwenye sekta mbalimbali za utumishi na uzalishaji na kutoa mchango muhimu sana kwenye maendeleo ya nchi yetu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa rai kwa uongozi wa CKHT na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TVV) wahakikishe kuwa udahili wa CKHT unatanuliwa kwa sababu hadi sasa chuo kina kozi moja tu ya maandalizi kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuingia kwenye Shahada. 

Waziri Mkuu amesema katika kuongeza udahili kwenye elimu ya juu, ameshauri wawe na kozi ama programu za maandalizi kwa wale wanaotaka kusoma stashahada na kwa wale wa cheti pia. 

Amesema matokeo ya programu hizo yataongeza ushiriki wa Watanzania wengi kwenye elimu ya juu. “Wito wangu kwa TCU nchini kuhakikisha inasimimia na kuongoza, kwa kushirikiana na CKHT katika uanzishwaji wa programu hizi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora wa elimu ya juu.”

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 698 walitunikiwa vyeti wakiwemo 20 wa Shahada za Uzamivu (PhD) na wengine 185 Shahada na Stashahada za Uzamili, wengine 344 walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 166 walitunikiwa Stashahada na Astashahada mbalimbali. 

Mahafali hayo yamehudhuliwa naWaziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Mizengo Peter Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Chuo Mkoani Lindi Godfrey W. Zambi,

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania, Profesa Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania Profesa Elifas Tozo Bisanda na wakuu wa wilaya za mkoa wa Lindi

No comments:

Post a Comment

Pages