HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 31, 2020

MAPENZI KWA FAMILIA KIKWAZO CHA KUWEKEZA

 Mkurugenzi wa Masoko UTT AMIS, Daud Mbaga.
 
Chips Kuku.

 

Na Mwandishi Wetu



FAMILIA za Kiafrika mara nyingi zimekuwa na wanafamilia wasiopungua wanane. Hiyo ni staili ya maisha hasa pale  inapukuwa na ahueni ya kipato japo kidogo.



Idadi hiyo ya watoto kwa jamii za Afrika inazingatia majina ya pande zote kike na  kiumeni.

Utakuta familia kama hizo zina utamaduni wa kudekeza watoto,  utasikia ‘kanunueni chipsi kuku,’ baada ya kueleza kwamba ‘sisi hatupendi ugali, maharage, mchicha na mtindi.’

Maharage ndio usiseme kabisa, utamsikia mama akiwauliza watoto sasa mtakula nini? jibu rahisi la watoto utawasikia wakisema chipsi kuku au chipsi zege (mayai) na kuku.



Kwa sasa kilo ya unga shilingi 1,000, mnakula wote tena zaidi ya mlo mmoja, chips kuku shilingi 5,000 au zaidi na hamuwezi kula wote. Mkiwa zaidi ya watu 8, chipsi mayai na kuku ni pesa nyingi, mkila mara kwa mara ni pesa nyingi zaidi.

Fedha hizo zingeweza kuwekezwa na kutumika kununua unga wa ugali na maharage, mchicha na mtindi ni bora zaidi kuliko chipsi kuku. 

Unapokula chipsi, mayai na kuku kila mara, muda nao hausubiri, kadri unavyokwenda uzee nao unabisha hodi.

Kama ulizaa watoto miaka kadhaa iliyopita, watoto hao wanatakiwa kwenda sekondari au chuo. Umri wa mzazi unakwenda na kuwa watu wazima zaidi ambao kimsingi watahitaji uangalizi.



Fedha zote zikiishia kwenye chips kuku bila kufikiri kesho yake changamoto kubwa, chipsi, mayai na kuku imeleta shida katika familia nyingi na mwisho wa siku kusababisha umaskini.



Ukiwa kwenye umri wa kati inabidi uhudumie watoto na familia, inawezekana wazazi wako pia wanakutegemea, hizi ndizo tamaduni za familia za Kiafrika.


Vuta pumzi twenda pamoja, chunga pesa zako, kumbuka kuna midomo mingi inahitaji uilishe na si kulisha tu lakini na shida zingine za maisha kama mavazi, maradhi hata malazi.



Mambo mengine zaidi ya hayo ni pamoja na kwenda ufukweni, mgahawani na shida za ki ukoo. Afrika mtoto wa mwenzio ni wako pia.



Tukiwa kwenye ndege kukawa na dhoruba marubani na wahudumu wanasisitiza ujiwekee mwenyewe hewa ya ‘oxygen’ baada ya hapo ndipo umwekee na jirani yako ili naye aweze kupumua.

Kwa maneno mengine ni kwamba, anza na wewe mwenyewe kwanza halafu jirani afuatie, jirani anaweza kuwa baba yako, mwanao hata dada au kaka yako wa kuzaliwa tumbo moja.



Mfano kama una madeni, unahangaika kukidhi mahitaji yako muhimu utayari wako wa kusaidia watu wengine kifedha unakuwa bado, inabidi wasubiri, pengine muda mrefu.

Kwa kipato chochote unachopata jaribu kuweka kiasi hata kidogo kwa ajili ya dharura, lipa madeni yako kwa mpangilio maalum, weka kiasi hata kidogo kama akiba ya uzeeni huku ukikumbuka iko siku watoto wataenda sekondari au chuoni, pamoja na ugumu wa maisha pambana na hali yako.



Wanaokuzunguka waambie ukweli kuwa huwezi kuwatimizia, acha wakuchukie lakini kama ni chipsi kuku wajifunze kutafuta kwa jasho lao.

Wale wanaokutegemea waende kwa bajeti yako si kwa matamanio yao, wabane waambie ukweli ili uweze kupata ziada kwa ajili ya uwekezaji.



Wanaoweza kufanya kazi watafute hata vibarua, mfano wakati watoto wanasubiri matokeo ya mitihani na nyakati za likizo au baada ya kumaliza chuo ili waongeze pato la familia.

Kwa kuwa tatizo ni pesa na jinsi ya kuitengeneza, tuongelee pesa mara kwa mara katika usawa wa familia zetu.

Uliza kama watoto, ndugu chini ya familia yako wana madeni na yalikuwa ya nini? Je, kila mtu ana bima ya afya maana maradhi yatakutoa kwenye malengo yako, pesa yote inaweza kuishia kwenye matibabu ya kutibu maradhi.



Kama huna Bima ya Afya unaweza kutumia hadi thumuni ya mwisho na pengine ukaingia hata kwenye madeni badala ya kuwa mwekezaji ukawa fukara wa kutisha.

Kwa watoto waambie ukweli kuhusu maisha, waambie maisha si rahisi na si chipsi, mayai na kuku ila yaweza kuwa rahasi kama watakuwa wawekezaji, kuwekeza sehemu sahihi kama kwenye Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ya UTT-AMIS.



Mifuko hiyo, hata unapokuwa na pesa kidogo unaweza kuwa mwekezaji na ukawekeza mara kwa mara kadri unavyopata na inatoa faida jumuishi hivyo mtaji wako na faida kuwa vizuri kadri miaka inavyosonga mbele.

Ukifanya hivyo utakuwa umewapa watoto wako upendo wa kweli na si chipsi, mayai na kuku. Kila mtu ni muhimu, hakuna mwenye umuhimu kama baba, mama na watoto.



Mbali na umuhimu huo, kila jambo lina mtizamo na ufumbuzi tofauti kwani usipoangalia utatuzi kwa umakini wapendwa wako kama hao wanaweza kuwa chanzo cha mdororo wako kiuchumi.



Kama wanaokutegemea sana, kaa panga nao angalia mpango upi utakuwa mzuri na utakuwezesha kuendelea na maendeleo yako ya kiuchumi vinginevyo mtakufa wote.



Ondoa hisia, angalia kila jambo kiuhalisia, tumia mifano halisi ambapo kwa kufanya hivyo si ukatili ni kwa nia njema kwani uchumi wako ndiyo uchumi wao.

Wekeza kwa bidii, pia ni vizuri kuanza kuwekeza ukiwa bado kijana, kumbuka kuna siri kubwa kati ya uwekezaji na muda hasa unapopata faida jumuishi Katika Mifuko UTT-AMIS.



Kumbuka japo thamani ya kipande inapanda na kushuka au inaendeana na thamani ya mifuko bado ukianza mapema utakuwa vizuri kiuchumi miaka ya mbele.

‘Ukiwekeza sh. 200,000 kwa mwezi utakuwa umeweka sh.  24,000,000 kwa miaka 10. 

Kama pesa hizo zitakuwa kwa riba ya asilimia 10 kwa mwaka utakuwa na sh. 40,968,995.78.

“Kama riba ikawa asilimia 12, uwekezaji wako utakuwa sh. Milioni 46,007,737.9 ndani ya miaka 10. 

Kama uwekezaji huo ukawa wa miaka 20, utakuwa umeweka sh. 48,000,000 kwa asilimia 10 utakuwa na sh.151,873,767.20 kama asilimia ni 12 utakuwa na sh. 197,851,073.08,” anafafanua Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT- AMIS, Daudi Mbaga.



Anasema hayo ndiyo maajabu ya uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Kumbuka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inasisitiza kueleza ukweli kuwa thamani ya kipande inaweza kupanda au kushuka.

Kumbuka kupanda na kushuka kwa thamani ni tabia ya uwekezaji wote, hata ungekuwa na duka, hoteli kuna siku unapata zaidi na kuna siku unapata kidogo kwa uwekezaji huo huo au pale unapokuwa umeongeza mtaji.



Ni muhimu jamii ikatambua kuwa kuna dharura, hivyo weka fungu la dharura, ikishapatikana wekeza la malengo ya baadaye ikiwemo kustaafu, malengo ya kustaafu yanatakiwa yaanze siku ya kwanza unapoanza kazi, punguza chipsi, mayai na kuku.



Mbaga anasema malengo ya baadaye sio kustaafu tu, elimu kwa watoto nayo imo, fikiria wakifika chuo itakuwaje, wakifikisha miaka ambayo wanaweza kufanya kazi wasome huku wakifanya kazi ambayo si lazima iwe ya ajira.

Mfano, nyumbani mnaweza mkawa mnafuga mifugo kama kuku, ng’ombe, mbuzi na mingine, badala ya kuaajiri mtu wa kuhudumia mifugo hiyo ni vizuri watoto wakapangiana zamu.



Pesa ambayo ungemlipa mfanyakazi kwa kazi hiyo inaweza kuwekezwa kwa maisha ya baadaye, kumbuka shilingi milioni 1 ikikaa ndani ya uwekezaji miaka 30 kwa kwa asilimia 15 itakupa shilingi milioni 66 je, ingekuwa milioni mbili, tatu, nne, wakati wa likizo ndefu watoto wanaweza ongeza tija zaidi.

Watoto waishi kwa gharama za bwalo za chuo na si kwa chipsi, kuku na mayai.

 Hii itawasaidia kuishi maisha halisi na si maisha ya kuiga baada ya chuo.

Ili uweze kuwekeza, wapeleke watoto shule ambazo unaweza kumudu gharama zake, kwa mfano hapa nyumbani kuna tofauti kubwa kati ya shule za serikali na binafisi.

Kama wewe ni msomi kidogo si lazima upeleke watoto twisheni, unaweza kumfunza mwanao wewe mwenyewe au kumpa ushawishi wa kujiunga kwenye kundi la wale wanaofaulu vizuri darasani na kusoma pamoja.



Kwa kufanya hivyo utatengeneza fungu ambalo utaweza kuliwekeza kwenye mifuko ya UTT AMIS au kwingineko.

Mbaga anafafanua kuwa, makala hii imejikita kwenye kupunguza anasa (chipsi, kuku na mayai) kama mfano, pia imeelezea kirefu jinsi gani mapenzi kwa watoto, wazazi, mke yanaweza kuifanya ndoto yako ififie kwenye uwekezaji.



Nafahamu ni vigumu kuwaambia wazazi, pengine hata watoto hapana lakini ili mipango ya pesa iwe ya uhakika inabidi uwe na uwezo wa kukataa jambo fulani ambalo usipolifanya litaleta unafuu katika maisha yako na wao hapo mbele ya safari.

Kumbuka kuwasaidia si kuwapa pesa, nenda nao kanisani, msikitini, shamba, wasaidie katika mipango yao, watoto wape maarifa ya maisha wasiwe na akili za darasani pekee.



Kwa wazazi tumia mbinu mbalimbali wakuelewe kwani kwa miaka mingi wao walikuwa wameshika usukani sasa unajaribu kuchukua nafasi yao, waswahili wanasema mtoto kwa mama hakui.

Kama kuna madeni lazima yalipwe tena kwa mpangilio maalum kwani kuwa mwekezaji ukiwa na madeni makubwa tena yenye riba za juu inaweza kuwa tabu.

Riba huongeza ukubwa wa deni kama faida jumuishi inavyokuwa kwenye riba inayoingia kwa mfuko wako.



Tumezungumza kuwa upendo mzuri kwa familia sio chipsi, mayai na kuku ila kuwekeza ndo upendo wa kweli, uwekezaji utatupa pesa nyingi zaidi na pesa ndiyo kila kitu, wahenga wanasema pesa sabuni ya roho.



Tufanye nini sasa ili twende pamoja katika safari yetu ya uwekezaji, jambo la kwanza ni kupunguza ugomvi wa fedha

Ni vigumu kukwepa ugomvi wa fedha kati ya mke, mume na pengine hata ndugu ikiwemo wazazi. 

Ugomvi wa pesa pengine umefanya hata ndoa au familia kusambaratika.

Bajeti yaweza kuwa vita na hapa ni pale, mahitaji hayawiani na kila mtu anaona hitaji lake ni muhimu zaidi ya mwenzake na pale ambapo kila mtu ana bajeti kivyake.

Kumbuka mkibajeti pamoja ni kama mnawekeza pamoja sababu kila mtu anachangia hivyo, fungu la fedha za kutumia pamoja  linakuwa kubwa.



Fedha ikiwa nyingi unaweza fanya jambo ambalo awali ulikuwa huwezi kulifanya, miamala inakuwa rahisi na nguvu ya kujadili bei na vitu vingine inaongezeka.

Inabidi kukaa uso kwa uso na kujadiliana tena kiungwana juu ya matumizi yenu kwa pamoja. Mkubaliane tofauti zenu, kumbuka kila binadamu yuko kipekee, hakuna jinsi yeyote ile utakuta watu wawili wanafikiri sawa, na wana tabia sawa.



Hata mapacha hutofautina. Kila mtu aweke shida zake kando na fikra zenu ziende sawa, jaribu kuwa na mtizamo mmoja.

Kwepeni kukuza na kuchanganya mambo, viapo kama siwezi thubutu kufanya jambo hilo au kauli kama kila siku unanionea inaleta kinyongo na historia kuwa mwaka jana ulifanya hivi, mwaka huu unarudia tena, ikiwa hivyo hamuwezi kusonga.



Mtofautiane kwa maendeleo, mgombane kwa maendeleo ya kiuchumi na kifamilia. Ugomvi usifute mafanikio au makubaliano mazuri ya awali. Kumbukeni pesa ni sabuni ya roho, ugomvi unauma na unachosha akili.

Tunashauriwa kuwa na akaunti za pamoja lakini kushirikiana kwenye kila senti ni jambo gumu sana kwa wanandoa kwani kila mtu ana matumizi yake binafsi.



Ni vizuri kukubaliana ni kiasi gani kiwekwe pamoja, asilimia ngapi kila mtu abaki nayo kwa ajili ya matumizi binafsi.

Kiasi cha matumizi binafsi ni huru kwa kila mweza kukitumia vile atakavyo bila kuulizwa, hii inatoa uhuru wa kutumia bila uoga kwenye shida au matumizi binafsi.



Kwa mujibu wa Mbaga, usimamizi wa bajeti uwe wa pamoja, hapa haijalishi kama mmoja anafanya kazi na mwingine hafanyi.

Ni muhimu kujadili pamoja kipi kifanyike na ni kipi kisifanyike au kisubiri kwanza. Bila kufanya hivyo na kama hakuna uwazi kutoaminiana kutaibuika.



Kumbuka mmekutana ukubwani kila mtu ametoka kwake, tunaambiwa tusifichine mambo, tusiwe wasiri lakini ikija kwenye swala la hela inakuwa changamoto kubwa sana.



Cha muhimu ni kupanga pamoja kwa sabubu ugomvi wa pesa na changamoto zake hauishi, kila bili zikija unaibuka, lipa wewe, nimechoka kulipa kila siku.

Kama lengo ni kujenga familia na pesa ndiyo inawatenga ni bora mfikiri mara mbili.

Ushauri pangeni pamoja matumizi ya kila siku, fungu la dharura, uwekezaji kwa ajili ya maisha ya mbele.

Haya yawe mambo muhimu katika mpango wenu wa pamoja, kumbuka UTT AMIS ni kampuni ya serikali, njoo tuongee tukatae umaskini, njoo tuwekeze.



No comments:

Post a Comment

Pages