Mkuu
wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula eneo la Mgogoro wa ardhi lililopo
Kagunguli Ukerewe mkoa wa Mwanza.
Na Munir Shemweta, WANMM UKEREWE
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza kufanyika utambuzi wa mipaka sambamba na
kuweka alama katika eneo lenye mgogoro wa ardhi kati ya Kanisa Katoliki,
wananchi na shule ya msingi ya Kagunguli iliyopo wilaya ya Ukerewe mkoa wa
Mwanza
Uamuzi
huo unafuatia
kuibuka mgogoro kati ya Mapadri wa Kanisa Katoliki na Mkuu wa Wilaya ya
Ukerewe
Cornel Magembe kuhusu umiliki wa sehemu ya eneo la shule ya msingi
Kagunguli jambo lililosababisha Mapadri kuandika waraka wa
kutoshirikiana
na mkuu huyo wa wilaya.
Akizungumza katika
kikao cha utatuzi wa mgogoro huo uliohusisha Mapadri, Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya na Serikali ya Kijiji jana
wilayani Ukerewe mkoani Mwanza Dkt Mabula alisema maamuzi yote yaliyotolewa nje
ya utaratibu kuhusiana na mgogoro huo ni batili na usubiriwe utambuzi wa mipaka
ya eneo lenye mgogoro.
‘’ Wizara itatuma timu
ya wataalamu ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro kwa kubainisha na kutambua mipaka
ya hapa eneo Kagunguli na kuja na ufumbuzi wa kudumu’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza kupatiwa barua za maeneo yote ya
taasisi za dini yenye migogoro mikubwa ya ardhi ili iweze kushughulikiwa na
kubainisha kuwa katika kuishughulikia migogoro hiyo timu ya wataalamu itatumwa
katika maeneo husika kwa lengo la kubainisha uhalali wa pande zenye migogoro.
Alimtaka Mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Estar Chaula kujiandaa kugharamia wataalamu watakaokwenda
kubainisha mipaka yenye mgogoro katika halmashauri yake kwa kuwa halmashauri
ndizo zenye jukumu la kupanga maeneo yake.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema
kitakachofanywa na wizara yake sasa kuhusiana na mgogoro huo ni kwenda kufufua
mipaka na kuanisha matumizi ya eneo hilo ambapo alisisitiza kuwa ni vizuri maeneo
yote ya umma yakawekewa mipaka yenye alama zinazoonekana.
Mkuu wa wilaya ya
Ukerewe Cornel Magembe aliweka wazi kuwa, mgogoro uliopo katika eneo linalohusisha
shule ya Sekondari Kagunguli inayomilikiwa na Kanisa Katoliki umechochewa kwa
kiasi kikubwa na Mkuu wa shule ya Sekondari Kagunguli Padri Johanes Nawachi kwa
kile anachodai padre huyo eneo la shule yake kuvamiwa.
Hata hivyo, Magembe
alisema katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo aliagiza Kanisa Katoliki
kuwasilisha Hati ya umiliki eneo lake, huku serikali ya kijiji nayo ikitakiwa
kuwasilisha muhtasari wa kijiji kuhusiana na kutolewa sehemu ya eneo sambamba
na nyumba tatu za walimu wa shule ya msingi Kagunguli kubaki kama zilivyo ndipo
afanye maamuzi kuhusiana na mgogoro huo.
Alisema, kilichofanywa
na Mapadri wa Kanisa Katoliki kuandika waraka wa kutoshirikiana naye ni uchochezi
kwa waumini wa kanisa hilo na serikali na kubainisha kuwa hali hiyo
imesababishwa na msimamo wake wa kuhakikisha maeneo ya serikali yanalindwa.
Kwa upande wake Mkuu wa
Shule ya Sekondari ya Kagunguli Padri Johanes Nawachi alisema kumekuwa na
mahusiano mabaya baina yake na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe baada
ya kuanza zoezi la kupanda miti eneo alilodai kumilikiwa na kanisa Katoliki na
kuhusisha pia maeneo ya nyumba tatu za walimu wa shule ya msingi Kagunguli.
No comments:
Post a Comment