Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi itaanza kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote sugu wa kodi
ya pango la ardhi kuanzia kesho (tarehe 23 Machi 2020) katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwa ni jitihada za Wizara hiyo kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi
wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi wa kuwafikisha
mahakamani wadaiwa hao unafuatia kushindwa kulipa madeni yao hata baada ya
kupelelekewa ilani ya madai inayowataka kulipa madeni ya Kodi ya Pango la Ardhi
ndani ya wiki mbili baada ya kupokea hati ya madai.
Malengo ya Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya shilingi
bilioni 180 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya ardhi. Vyanzo hivyo ni Kodi
ya Pango la Ardhi, Ada za Upimaji Ardhi, Usajili wa Hati na Nyaraka pamoja na Ada
zinazotozwa kupitia Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba ya Wilaya.
Takriban wiki mbili
sasa Maafisa kutoka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Watumishi walioko
mikoani wamesambazwa maeneo mbalimbali nchini katika operesheni maalum ya kusambaza
ilani za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.
Akizungumza katika
mahojiano maalum leo tarehe 22 Machi 2020 jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha
Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami alisema uamuzi
wa kuwafikisha Mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi unatokana na
wadaiwa hao kushindwa kulipa madeni yao hata baada ya kupelekewa ilani za madai.
Alisema siku ya kesho (tarehe
23 Machi 2020) jumla ya mashauri 847 yatapelekwa katika Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba
ya wilaya katika mikoa ya Dar es Salaama, Mwanza na Lindi.
‘’Kesho tutapeleka
Mashauri 847 katika Mabaraza ya Ardhi katika mkoa wa Mwanza mashauri 450, Lindi
121 na Dar es Salaam Ilala 200 na Temeke 76 na lengo hapa ni kuhakikisha
tunakusanya kodi yetu ya pango la ardhi kama sheria ya umiliki ardhi
inavyoelekeza’’ alisema Masami.
Mkuu huyo wa Kitengo
cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, zoezi la
kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ni endelevu na kuwataka wamiliki
wa ardhi waliopewa ilani za madai kuhakikisha wanalipa madeni ndani ya wiki
mbili na kushindwa kufanya hivyo kutasababisha kufikishwa kwenye Baraza la
Ardhi la Nyumba la Wilaya na huko maamuzi yake ni kupigwa mnada mali za mdaiwa kufidia
deni.
Wakati wa uzinduzi mkakati
maalum wa Wizara ya Ardhi wa kuongeza maduhuli ya serikali kupitia kodi ya
pango la ardhi uliofanyika jijini Dodoma hivi karibuni, Kamishna wa Ardhi Nathaniel
Nhonge aliwaeleza Watendaji wa serikali za mitaa wakiwemo Wenyeviti kuwa wizara
yake itaanza kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo
yote nchini.
Alisema, opresheni hiyo
itaendeshwa na Maofisa wa Wizara ya Ardhi, watendaji wa sekta ya ardhi katika
mikoa na halmashauri kwa ushirikiano na Wenyeviti Mitaa ili kurahisisha kuwafikia
wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya ardhi kwa wakati
Aliwataka watendaji wa
serikali za mitaa na wenyeviti kushiriki kikamilifu katika operesheni hiyo sambamba
na kusimamia uendelezaji maeneo kutokana na jukumu hilo kuwa kwao na kubainisha
kuwa, kushindwa kuendeleza jukumu hilo kutasababisha migogoro ya rdhi na miji
kuendelezwa kiholela.
No comments:
Post a Comment