HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 01, 2020

BURIANI MARIN HASSAN WA TBC, KUZIKWA MWANAKWEREKWE KESHO

DAR ES SALAAM, TANZANIA

NGULI wa habari na mtangazaji mahiri wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Marin Hassan Marin (pichani), aliyefariki dunia leo Aprili 1, jijini Dar es Salaam, anatarajia kuzikwa kesho Alhamisi Aprili 2 kwenye Makaburi ya Mwanakwerekwe, visiwani Zanzibar.

Marin Hassan, amefariki dunia leo Aprili 1, 2020 katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam, alikokimbizwa na majirani baada ya kulalamika kutojisikia vema mapema leo asubuhi. Taarifa za kifo chake, zilithibitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Martha Swai.

Mkongwe huyo aliyezaliwa mwaka 1972, alikuwa jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kipindi chake cha Ardhio cha TBC1, uliofanyika Machi 30, kabla ya kushiriki kipindi hicho Machi 31, ambako aliondoka studio za TBC Mikocheni akiwa mzima wa afya saa 3:30 usiku.

Rais John Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa TBC na familia ya marehemu Marin, ambako ametoa ndege binafsi ya Rais, iliyofuata baadhi ya wana familia mjini Dodoma, kisha kwenda Dar es Salaam kuchukua mwili wa marehemu kuupeleka Zanzibar kwa maziko.

Habari kutoka nyumbani kwa marehemu Kibweni mjini Zanzibar, zinaeleza kuwa mipango ya maziko inafanyika na mazishi ya nguli huyo yanatarajia kufanyika Alhamisi, Aprili 2, majira ya saa 4 asubuhi, kabla ya sala ya Adhuhur, huko Mwanakwerekwe.

No comments:

Post a Comment

Pages