Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
akizungumza katika kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji maamuzi ya
kutoondolewa vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa katika mgogoro wa hifadhi kutoka
kwa makatibu wakuu wa sekta husika jijini Dodoma.(Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa kina
utakaoshirikisha sekretarieti za mikoa katika utekelezaji maagizo ya kutoondolewa
vijiji 920 vilivyokuwa na mgogoro maeneo ya hifadhi nchini.
Lukuvi alitoa maagizo
hayo jana jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya Makatibu Wakuu iliyowasilishwa
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kwa
Mawaziri wa Wizara zinazohusika katika utekelezaji huo kufuatia uamuzi wa Rais
John Pombe Magufuli kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 kwenye maeneo ya hifadhi
yaliyokuwa na mgogoro.
Wizara ambazo Makatibu
Wakuu wake wanashiriki kazi ya utekelezaji maagizo hayo ni Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Maliasili na Utalii, Kilimo, Maji, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Makamu wa Rais ambazo
Mawaziri wake walitembelea maeneo yenye mgogoro na kuja na mapendekezo
yaliyopelekea Rais kuchukua uamuzi huo.
Awali wananchi
waliokuwa wakiishi kwenye vijiji vya hifadhi ya misitu walionekana wavamizi
wakati serikali ilitoa hati za usajili kwa vijiji na wananchi wake kushiriki shughuli
mbalimbali zikiwemo za uchaguzi jambo lililomfanya Rais Magufuli kuchukua
uamuzi wa kuvibakisha vijiji 920 baada ya kupata ushauri wa mawaziri wa sekta
husika.
Lukuvi alisema, katika
kipindi hiki ambacho kamati za wataalamu zinapitia taarifa za utekelezaji
maamuzi kuhusiana na suala hilo lazima ufanyike uchambuzi wa kina ili kuja
majibu yatakayokidhi malengo ya uamuzi uliofanyika hasa ikizingatiwa baadhi ya maeneo
ya vijjiji hayahitaji kupunguzwa.
‘’Ufanyike uchambuzi wa
kina kuona faida itakayopatikana na vijiji vingapi vitanufaika na tupate taarifa
itakayoainisha kila eneo na makubaliano yake’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi,
kila sekta inayohusika inatakiwa kufanya uchambuzi katika eneo lake na kutolea mfano
Wizara ya Viwanda na Biashara inaweza kuja na uchambuzi utakaoainisha maeneo ya
EPZA yaliyorudishwa kwa wananchi huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikiainisha maeneo
yaliyopunguzwa kwa shughuli za ufugaji na kilimo na Kamishna wa Ardhi akibainisha
maeneo yaliyofutwa.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi
alisema wakati wa utekelezaji kazi ya uchambuzi ikiendelea wasimamizi wa sheria
katika maeneo ya hifadhi wanapaswa kuendelea kusimamia sheria na
kuwatahadharisha kuwa makini wakati wa utekelezaji majukumu yao ili kuepuka
uvunjifu wa amani.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema kamati ya Makatibu
Wakuu imeendelea kufanyia kazi utekelezaji maamuzi ya vijiji 920 kama
walivyoelekezwa.
Kwa mujibu wa Mary, kamati
ya Makatibu Wakuu katika kutekeleza maagizo ya Mawaziri inatarajia kukamilisha kazi
ya tahmini ya vijiji 920 katika muda wa wiki mbili na kuwasilisha taarifa yake kwa
mawaziri wa sekta kama ilivyoelekezwa mwisho wa mwezi huu wa Aprili.
Kwa muda mrefu wananchi
wa Vijiji 975 vilivyo katika hifadhi wamekuwa katika mgogoro kwa kudaiwa kuwa
wavamizi na kusababisha nyumba zao kuchomwa moto huku baadhi yao wakiwa
wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka ishirini.
Mgogoro huo ulisababisha
Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati na kuridhia vijiji 920 kubaki maeneo ya
hifadhi sambamba na kufutwa misitu ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715
ili ipangwe upya. Pia Rais Magufuli alifuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa
ekari 707,659.94 na ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo
na shughuli za ufugaji.
No comments:
Post a Comment