Mhandisi
Mkazi Haruna Kalunga (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo (mwenye kaunda suti nyeusi) katika eneo la ujenzi
wa Vihenge.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia na kusafisha mahindi vya NFRA katika eneo la viwanda kata ya Ntendo manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia na kusafisha mahindi vya NFRA katika eneo la viwanda kata ya Ntendo manispaa ya Sumbawanga.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amewatahadharisha mafundi na
vibarua wa mradi wa ujenzi wa vihenge unaojengwa na serikali ya Tanzania
kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kuwa makini na
ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona kwa
kufuata maelekezo ya wataalamu afya wawapo katika eneo la kazi na
wanaporudi kwenye familia zao.
Amesema
kuwa afya ya kila mmoja ni muhimu kutokana na mchango wake katika
kujenga nchi na hivyo kuwataka kuwa makini kwa kunawa kila mara hali
iliyopelekea kumuagiza meneja wa mradi huo kwa niaba ya Wakala wa
majengo nchini (TBA) Mhandisi mkazi Haruna Kalunga kuhakikisha eneo hilo
la kazi kunakuwa vifaa vya kutosha vya kunawia maji na sabuni kwa
kukanyaga kwaajili ya wafanyakazi na kuondoa ndoo zilizopo ambazo koki
zake hazina usalama.
“Afya
yako ni ya Msingi sana, na familia yako na sisi sote kwa ujumla wake,
kwa maana wewe mtu mmoja ukiugua Corona utaweza kuusambaza kwa watu
wengi sana, na wote hapa mnaweza mkafutika ndani ya wiki moja tu, sasa
mtakuwa mmeiweka nchi mahali pabaya na mradi wenyewe utasuasua, kwahiyo
mjihadhari na ugonjwa huu hatari wa Corona, lakini mchape kazi msiogope
kuchapa kazi,” alisema.
Aidha,
alitoa pongezi kwa mkandarasi wa mradi huo Unia araj kutoka nchini
Poland kwa kusaidiana na mkandarasi mzawa Elerai kutoka Arusha pamoja na
meneja wa mradi huo TBA pamoja na mafundi wa mradi huo kwa kufanya kazi
ndani ya wakati mbali na hali ya hewa kutokuwa Rafiki kwa ujenzi huo na
hivyo kuwataka kuongeza kasi ili kukamilisha ujenzi huo ifikapo tarehe
9.3.2021.
“Ningependa
ratiba hiyo izingatiwe, tusirudi nyuma tuongeze kasi kwa kiwango
ambacho mradi huu tunataka umalizike mapema, utakuwa na manufaa makubwa
sana kwasababu uwezo wa kutunza nafaka zetu kimkoa utaongezeka kutoka
tani 30,500 za sasa mpaka kufika tani 55,500 utakuwa ni uwezo mkubwa,
kwahiyo hata wakulima wetu watahamasika kulima mahindi zaidi wakijua
kwamba NFRA itaweza kuyanunua na kuyahifadhi kwa matumizi ya ndani na
nje ya nchi,” Alisema.
Kwa
upande wake Meneja wa Mradi wa TBA Mhandisi Mkazi Haruna Kalunga
alisema kuwa ujenzi huo utajumuisha majengo 13 ambapo ujenzi wa vihenge 6
vikubwa na vihenge 2 vidogo pamoja na miundombinu yake itachukua
asilimia 70 ya mradi huku asilimia 30 ikibebwa na majengo saidizi.
“Kuna
Jengo la utawala, kuna jengo la kupikia na kulia chakula, kuna jengo la
kutunzia vifaa na dawa, kuna jengo la maabara kwaajili ya upimaji wa
hizo sampuli ambazo zitakuwa zinaingia hapa, kuna vihenge 6 vikubwa na
vihenge vidogo kwaajili ya usafi vyenye jumla ya tani 20,000 na pia tuna
ghala la kuhifadhia mazao lenye uwezo wa kubeba tani 5,000,” alisema.
Kwa
mkoa wa Rukwa mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani 6,019,399.00
wakati mkandarasi huyo akifanya kazi katika mioa mingine ya Manyara na
Katavi ambapo jumla ya gharama yake ni $20,280,906.00 ambapo hadi sasa
mkandarasi huyo ameshalipwa $ 10,175,714.22.
No comments:
Post a Comment