Mwenyekiti wa Kamati ya
Amani Mkoa wa Songwe Sheikh Hussein Issa akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo
ambapo wamekubaliana kutoruhusu watoto katika nyumba za ibada ikiwa ni hatua mojawapo
ya tahadhari zaidi juu ya ugojwa wa Corona.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akishiriki kikao cha kamati ya Amani Mkoa ambapo
amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuhakikisha anatoa elimu ya tahadhari
ya Corona katika nyumba zote za Ibada.
Na Mwandishi Wetu
Katika jitihada za kupambana
na Ugonjwa wa Corona, Chifu wa Mkoa wa Songwe Mbeshena Nzunda ametoa marufuku
kwa waganga wa jadi kupokea mgonjwa yeyote ambaye hana ripoti itakayo onyesha
tatizo husika limeshindwa kutatuliwa hospitalini.
Chifu Nzunda amebainisha
hayo katika kikao cha Kamati ya Amani ya Mkoa ilipokutana kujadiliana hatua zaidi
za tahadhari zinazo paswa kuchukuliwa na Mkoa wa Songwe ili kupambana na ugonjwa
wa Virusi vya Corona.
Amesema ili mgonjwa apate
matibabu kwa mganga wa jadi anapaswa kuonyesha ripoti kuwa baada ya kutibiwa
hospitalini hakupona na wataalamu wa
afya wathibitishe hilo pia waganga wa jadi wenye wateja wengi wanapaswa
kuwahudumia kwa awamu ili kepusha msongamano.
Chifu Nzunda ameeleza kuwa
waganga wa jadi wanatakiwa nao kuchukua tahadhari za Ugonjwa wa Corona kwa
kunawa mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni pia kuweka maji hayo kwa ajili
ya wateja watakao wahudumia.
Ameogeza
kwa kuwataka
watumiaji wa pombe za kienyeji kuhakikisha hawachangii vyombo vya
kunywea pombe
kama ilivyo zoeleka bali kila mmoja awe na chombo chake pia wauzaji
pombe hizo wachukue tahadhari kwa kuweka maji ya kunawa pia kupunguza
misongamano.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Amani Mkoa wa Songwe Sheikh Hussein Issa amesema kamati hiyo imekubaliana kuchukua
baadhi ya hatua ikiwa ni kuongeza tahadhari Zaidi ya Ugonjwa wa Corona huku
Uongozi wa Mkoa ukipongezwa kwa jitihada zilizochukuliwa hadi sasa hakuna
mgonjwa wa Corona.
Sheikh Issa amesema
kuanzia sasa watoto wasiruhusiwe kushiriki katika nyumba zozote za ibada ili
kuwaondoa katika hatari ya maambukizi ya Corona pia wazazi wahakikishe watoto
wanabaki majumbani.
Ameongeza kuwa nyumba zote
za ibada zisiruhusu waumini wengi kujaa bali waingie wachache na wakae mbalimbali
bil kusongamana pia maji tiririka ya kunawa na sabuni au vitakasa mikono viwekwe ndani na nje ya nyumba hizo za Ibada.
Sheikh Issa amesema
viongozi wote wa dini mbalimbali wanapaswa kuchukua tahadhari juu ya Ugonjwa wa
Corona kwa kufuata maelekezo ya Serikali pia wasiache kumuomba Mungu ili
ugonjwa wa Corona usilete maafa katika Nchi ya Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameipongeza kamati hiyo kwa hatua hizo za tahadhari
ya Corona huku akimuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuhakikisha anatoa
elimu ya tahadhari ya Corona katika nyumba zote za Ibada.
No comments:
Post a Comment