Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipimwa hali yake ya joto
la mwili kabla ya kuingia katika ofisi za kituo cha Uhamiaji kilichopo
katika mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia,uliopo
kata ya Itete, Wilayani Kalambo.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa, Joachim Wangabo, ameitaka Kamati ya maafa ya Mkoa kuhakikisha
wanaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa, Kata, Tarafa hadi Mkoa huku
akisisitiza mkazo wa kutolewa kwa elimu hiyo uelekezwe kwa vijana ambao wengi
wao wanaonekana kutofuatilia taarifa za habari pamoja na elimu mbalimbali
zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya ugonjwa wa Corona.
Amesema kuwa
vijana wa kisasa kuanzia mjini mapaka vijijini wamekuwa wagumu kusikiliza
taarifa ya habari kwenye redio wala kuangalia taarifa ya habari kwenye runinga
zaidi ya kujiendekeza kusikiliza muziki bila ya kujali na kutaka kujua serikali
inasema nini juu ya kujikinga na maradhi hayo ya Corona.
“Akitembea
kuna vitu viko masikioni humu anasikiliza muziki tu, nini serikali inasema
kuhusu janga hili hajui, lakini mambo haya yanazungumwa sana kwenye redio,
yanasemwa sana kwenye televisheni zetu, program ziko nyingi lakini vijana na
kundi kubwa wanaonekana hawana muda wa kufuatilia, tuwarudishe hili kundi kubwa,
lijenge tabia ya kufuatilia nini kinazungumzwa kwenye redio, kila redio inazungumza,
ziko redio za ndani ziko redio zenye sura ya kitaifa,” Alisisitiza.
Aliongeza
kuwa hii inaweza kuwa vita ya tatu ya dunia isipokuwa adui hatumuoni hivyo
hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake akaendeleza kutoa elimu bila ya kuchoka
ili kuweza kupambana na adui huyu ambaye haijulikani lini atashindwa.
Ameyaongea
hayo wakati alipofanya kikao na kamati ya maafa ya mkoa iliyowajumuisha waganga
wakuu wa wilaya wakiongozwa na mganga mkuu wa mkoa, viongozi wa dini na wataalamu
wa ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya jamii wa mkoa na taasisi zisizo za
kiserikali zinazojihusisha na kutoa elimu za afya katika mkoa.
Aidha,
Alisisitiza ili kuweza kufanikisha kufikisha elimu kwa wananchi wote wa mkoa
huo hakuna budi kuwaelimisha viongozi wa ngazi zote wakiwemo wenyeviti wote wa
vijiji na mitaa ili watilie mkazo utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika
maeneo yao ya kiutawala.
Kuhusu
ulinzi wa Mipakani Wangabo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa una vipengo 50 katika
ziwa Tanyanyika ambavyo hutumika na wananchi wan hi ya jirani ya Kongo na hivyo
kuwataka wananchi kuwa makini na wavuvi wote wanaotoka katika nchi hiyo
kuhakikisha wanawarudisha walikotoka na kisha kuripoti kwa vyombo vya usalama
na kusisitiza kuwa wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuwa walinzi wa kwanza wa
usalama wa nchi yetu.
No comments:
Post a Comment