Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni
Mstaafu, George Mkuchika (kushoto) baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021. Wa tatu kulia ni Waziri
wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga, kulia ni Waziri wa
Elimu, Sayansi na Tekinolojia , Profesa Joyce Ndalichako, na wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angelina Mabula. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekuwa
ikifuatilia utendaji kazi wa watendaji wake ili kuhakikisha kuwa hakuna
uzembe wa aina yoyote unatokea na kusababisha kuharibika kwa uchaguzi.
Amesema
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa,
zikisomwa pamoja na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya
Ushahidi na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma,
ikithibitika kuwa mtumishi husika ameharibu uchaguzi na kuisababishia
Serikali hasara, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kuachishwa kazi.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 6, 2019) Bungeni jijini
Dodoma kwenye mkutano wa 19 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi
ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema utaratibu upo wazi wa kushughulikia
watendaji wa uchaguzi wanaofanya uzembe wakati wa utekelezaji wa
majukumu yao kwani NEC hutekeleza majukumu yake kwa uhuru na bila
kufuata maagizo ya mtu yeyote.
“…kwa
mujibu wa Ibara ya 74(7) na (11) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikifanya kazi
zake kwa weledi na kwa kuzingatia maelekezo ya Katiba, Sheria, Kanuni,
Miongozo na Taratibu zilizopo.”
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa NEC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa
kuwashirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi, mfano, kabla ya kuanza
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ilikutana na wadau wa
uchaguzi katika ngazi ya Taifa na ngazi ya mikoa.
Amesema
wadau hao ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini,
wawakilishi wa Asasi za Kiraia, viongozi wa makundi maalum ya watu wenye
ulemavu, vijana, wanawake, wahariri na waandishi wa habari.
Waziri
Mkuu amesema lengo la ushirikishaji huo ni kuwataarifu kuhusu matakwa
ya kisheria ya kuboresha Daftari, kupata maoni yao na kuwajengea wadau
uelewa wa pamoja kuhusu uboreshaji.
Amesema
kupitia mikutano, wadau wote waliafiki kuhusu taratibu zilizowekwa na
Tume katika kutekeleza jukumu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura.
Pia,
Waziri Mkuu amesema vyama vya siasa vilielezwa haki ya kisheria ya
kuweka mawakala katika vituo vya uboreshaji wa Daftari na wakati wote wa
uboreshaji mawakala wa vyama mbalimbali walikuwemo vituoni.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema mwaka 2019/2020, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa ilichunguza na kuvitaka baadhi ya Vyama vya Siasa vilivyotuhumiwa
kuvunja katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa kuwasilisha maelezo
kwa Msajili. “Vyama hivyo, baada ya kutoa maelezo kwa Msajili, baadhi
yake vilipewa adhabu mbalimbali ikiwemo onyo.”
Amesema
katika kuhakikisha kuwa Vyama vya Siasa vinakidhi na kutekeleza matakwa
ya Sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajilli wa Vyama vya Siasa, Ofisi
inaendelea kuvifanyia uhakiki vyama vyote kuhusu utekelezaji wa
masharti ya usajili na matakwa mengine ya Sheria ya Vyama vya Siasa na
Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
No comments:
Post a Comment