Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN) Bruno Ghumpi (mwenye
shati la batiki) akitoa maelezo kuhusu umuhimu wa uwepo wa elimu kwa wazazi na
walezi ili kuwaelimisha watoto kuhusu kujikinga na maambukizi ya Virusi vya
Corona katika kikao kilichofanyika jijini.
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) kwa kushirikiana na Mtandao wa
Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN), Taasisi ya
Chakula na Lishe, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF)
wameandaa mkakati wa kufikisha ujumbe kwa watoto kuhusu kujikinga na maambukizi
ya Virusi vya Corona.
Akizungumza leo katika kikao kazi
kilichowakutanisha wadau hao jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa
Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN) Bruno
Ghumpi amesema kumekuwepo na ujumbe mbalimbali katika kujikinga na maambukizi
ya Virusi vya Corona ila kumekosekana ujumbe maalum unaolenga makundi maaalum
ikiwemo wanawake wajawazito na watoto wadogo kuanzia miaka 0 hadi minane.
Ameongeza kuwa kuwepo kwa elimu sahihi kwa watoto
hao kuhusu ugonjwa wa COVID 19 itawasaidia wazazi au walezi na watoto wenyewe
kupata taarifa zitakaziwasaidia kujikinga na Virusi hivyo ili kupunguza au
kuondokana na maambukizi ya Virusi hivyo katika maeneo yao.
“Ujumbe huu kwa watoto ni muhimu sana kwani kundi
hili kwa sasa lipo nyumbani kutokana na kufungwa kwa shule hivyo ni vizuri
wazazi na walezi wakazingatia masuala muhimu ya kuwafundisha watoto wao
kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona” amesema
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu
kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya
Maendeleo ya Jamii Bw. Mathias Haule amesema kuwa ni muhimu kwa wadau
kuhakikisha wanafikisha elimu katika ngazi ya chini kuanzia familia,
kijiji/mtaa ili kuwezesha watu hao kupata taarifa na elimu sahihi juu ya
kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
“Elimu ifike katika ngazi ya familia hasa katika
maeneo ya vijijini ambako bado elimu haijawafikia kwa kasi inayotakiwa ili
kuondokana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini.” Amesema
No comments:
Post a Comment