HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 10, 2020

TANZANIA YATOA BIILIONI 10 KUIFUFUA TAZARA

Muonekano wa moja ya Vichwa vya treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) vilivyokamilika baada ya kufungwa mashine ya kufua umeme (Tranction Motor), katika karakana ya Mamlaka hiyo Mkoni Mbeya.
 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Mbeya, Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, mara baada ya kukagua vichwa viwili vya treni ya shirika hilo vilivyofungwa mashine ya kufua umeme (traction motor) mpya.


Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Tanzania imetoa kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kufufua upya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuiongeza mtaji na kufikia lengo la kujiendesha kibiashara.

Utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa makubaliano ya nchi ya Tanzania na Zambia ambazo kwa pamoja zilikubaliana kutoa shilingi bilioni 20 ambapo kila nchi ilitakiwa kuchangia shilingi bilioni 10 ili kuifufua upya mamlaka hiyo na kuiwezesha kujitegemea mara baada ya kushuka kwa usafirishaji kutokana na upungufu wa vichwa.

Akizungumza mkoani Mbeya wakati akikagua vichwa viwili vilivyokamilika baada ya kufungwa mashine mpya za kufua umeme (traction motor), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema kuwa kukamilika kwa ukarabati huo kutaongeza usafirishaji wa mzigo kwa mamlaka.

“Makusudi makubwa ya Serikali kuwekeza fedha hizi ni kuhakikisha mnafanya biashara na kurejesha mzigo wa tani milioni tano mnaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka,” alisema Mhandisi Kamwelwe.

Kamwelwe alifafanua kuwa fedha hizo zilizotolewa zimeshanunua mashine mpya za kufua umeme takribani arubaini na mbili ambazo zitafungwa kwenye vichwa saba.

Meneja Karakana ya TAZARA mkoani humo, Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, alisema mpaka sasa vichwa viwili vimeshakamilika na mwishoni mwa mwezi huu kichwa cha tatu kitakamilika ambapo kichwa kimoja kina uwezo wa kusafirisha tani laki mbili na nusu kwa mwaka.

“Kukamilika kwa vichwa hivi kutaongeza mzigo tunaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka kwani kwa sasa mzigo tunasafirisha umepungua sana na hauzidi tani laki tatu, tunaishukuru sana Serikali kwa kuiwezesha mamlaka,” alisema Mhandisi Mong’ateko.

Mhandisi Mong’ateko aliongeza kuwa sambamba na ukarabati wa vichwa hivyo mkoani humo, Mamlaka inaendelea na ukarabati wa mabehewa katika karakana ya mamlaka jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha ukamilikaji wa vichwa hivyo unaendana na ongezeko la usafirishaji wa abiria na mizigo.

“Kukamilika kwa ukarabati wa vichwa hivyo kutaongeza idadi ya vichwa kumi na tatu vilivyopo kwa sasa na kufikia vichwa 20 ambapo kila kichwa kina uwezo wa kubeba tani elfu thelathini,” alisema

No comments:

Post a Comment

Pages