Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 4, 000,000,000/=
kutoka kwa Meneja Mkazi (Country Manager) wa Kampuni ya Madini ya
Barric - Twiga Minerals, Hilaire Diarra (kushoto) na Msaidizi wake,
Neema Ndossi (kulia) ukiwa ni mchango wa Kampuni hiyo kwa ajili ya
kuunga mkono juhudi za Serikali za mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa
kali ya mapafu- COVID - 19. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye viwanja
vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 8, 2020. Wa pili
kushoto ni Waziri wa madini, Doto Biteko na wa pili kulia ni Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.
Faustine Ndugulile. ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 1,000,000,000/=
kutoka kwa Mfanyabiashara, Rostam Aziz (wa tatu kushoto) ukiwa ni
mchango binafsi wa mfanyabiashara huyo wa kuunga mkono mapambano dhidi
ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID - 19.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na wadau mbalimbali
waliojitokeza kutoa michango kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serkali
za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID - 19 kwenye
viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 8, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja
na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya
mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya
sh. bilioni 6.226.
Baada
ya kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao kwa
kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya
corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa
huo nchini na wagonjwa watano wamepona.
Waziri
Mkuu amepokea msaada huo leo (Jumatano, Aprili 8, 2020) katika Ofisi
Waziri Mkuu Mlimwa, jijini Dodoma. Amewataka Watanzania waendelee
kushirikiana na Serikali katika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema
hadi sasa jumla ya watu 396 wapo kwenye karatini katika maeneo
mbalimbali yaliyotengwa wakiwemo wageni wanaoingia nchini ambao
wanafuatiliwa afya zao na baada ya siku 14 kama watakuwa hawana
maambukizi wataruhusiwa kuungana na familia zao.
Waziri
Mkuu amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali
katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye
utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya
corona.
“Serikali
inatoa misitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu
kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa
sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya
lazima.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee
kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae kwa sababu
hadi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi wa corona
nchini.
Pia,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo vya habari nchini
kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na
virusi vya corona pamoja na wasanii waliotunga nyimbo za kuuelimisha
umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Miongoni
mwa wadau waliotoa msaada huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa
sh. bilioni nne, mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh.
bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya
mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita 50,000 zitakazotumika
katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona nchini yakiwemo
magari ya kubebea wagonjwa.
Wengine
ni kampuni ya TEHAMA ya Huawei imetoa vifaa kuendeshea mikutano kwa
njia ya video ambavyo ni cloudlink camera tatu, Cloudlink Mic tatu,
Cloudlink TV terminal tatu, Cloudlink Platform pamoja na Thermal Imaging
Temperature Measuring System sita vyote vikiwa na thamani ya sh.
milioni 940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.
Baada
ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli
aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya
kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia
Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Kuhusu
wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake
iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote
wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.
Awali, mfanyabiashara
maarufu nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo
ameielekeza katika kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na
wasafiri wa daladala wa Dar es Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia
kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo kuweza kujikinga.
Pia,
Mfanyabiashara huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John
Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na
taharuki kama ilivyotokea katika mataifa mengine. Amempongeza Waziri
Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na corona.
No comments:
Post a Comment