Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.
Jen. Nicodemus Mwangela akipokea mchango wa shilingi 280,000 Kutoka kwa Mchungaji
John Mwasakilali Mkuu wa KKKT Jimbo la Magharibi (Songwe) kwa ajili ya mapambano
dhidi ya Ugonjwa wa Corona kwa Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela, akizungumza na viongozi wa KKKT wakati akipokea
mchango wa shilingi 280,000 kwa ajili ya mapambano ya Corona ambapo amewataka
wananchi kuchukua tahadhari kwa wageni
wanao ingia Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.
Jen. Nicodemus Mwangela akikabidhi mchango wa shilingi 280,000 Kutoka kanisa KKKT
Jimbo la Magharibi (Songwe) kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Hamad
Nyembea kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Corona.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Songwe kuchukua
tahadhari kwakuwa sasa kumekuwa na wageni wengi wanao ingia Mkoa wa Songwe
kutoka katika Mikoa mbalimbali hasa yenye wagonjwa wengi wa Corona.
Brig. Jen. Mwangela ameyasema
hayo mapema leo wakati akipokea mchango wa shilingi 280,000 Kutoka Kanisa la
Kiinjili la Kiluteri Tanzania Jimbo la Magharibi (Songwe) kwa ajili ya mapambano
dhidi ya Ugonjwa wa Corona kwa Mkoa wa Songwe.
“Kwa sasa Mkoa wetu
umeanza kupokea wageni wengi kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na hata Zanzibar, hatuwezi
kuwazuia kwakuwa nchi yetu ni moja lakini tusaidiane kutoa elimu ya Corona kwa
wageni hao na tuchukue tahadhari zote muhimu.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa kila
mwananchi akipata mgeni kutoka mikoa hiyo waangalie namna ya kutenga chumba kwa
ajili ya mgeni huyo ili asichangamane na watu wengine au kutoa taarifa kwa
uongozi wowote endapo watakuwa na mashaka na hali ya afya ya wageni hao ili
waweze kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Aidha amewapokeza Kanisa
la KKKT kwa kuwa taasisi ya dini ya kwanza kwa kuchangia mapambano ya Corona
kwa Mkoa wa Songwe pia kwa kuchukua tahadhari zote muhimu za kujikinga na
Corona ikiwa ni pamoja na kutoruhusu watoto wahudhurie ibada.
Brig. Jen. Mwangela
amesema taasisi za Dini ziendelee kuchukua tahadhari na kutoa elimu ya
kujikinga na ugonjwa wa Virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kuwatembelea
waumini majumbani mwao kuwapa elimu hiyo.
Naye Mkuu wa KKKT Jimbo la
Mgharibi (Songwe) Mchungaji John Mwasakilali amesema wanampongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John P. Magufuli kwa kutofunga shughuli za
ibada kwa makanisa hayo.
Mch. Mwasakilali ameongeza
kuwa wamechukua tahadhari ya kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa
kupunguza muda wa ibada hadi kufikia saa moja, kukaa kwa kuachiana nafasi na
kunawa kwa maji tiririka na sabuni na kuwa waumini wake wametii maelekezo ya
Serikali.
Ameongeza kwa kuipongeza
serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kama tahadhari ya kuwakinga wananchi dhidi
ya ugonjwa wa Virusi vya Corona nao wataendelea kuunga mkono jitihada za
serikali kwa kufuata maelekezo na kwa michango mbalimbali pale inapobidi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema fedha hizo zilizotolewa na kanisa la KKT
zitasaidia kununua baadhi ya vifaa vinavyohitajika katika Kituo cha Afya
Nanyala ambacho kimeteuliwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa ngazi ya Mkoa endapo atapatikana
Mgonjwa wa Corona.
Dkt Nyembea ameongeza kwa
kuwaomba wadau waendelee kujitokeza
kuchangia mahitaji mbalimbali kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona
kwakuwa Vita ya Ugonjwa huo inahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
No comments:
Post a Comment