Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.
Jen. Nicodemus Mwangela akipata maelezo ya namna ambavyo wasafiri wanaotumia mpaka
wa Tunduma hupimwa endapo wana maambukizi ya Virusi vya Corona kabla ya
kuruhusiwa kuingia nchini.
Na Mwandishi Wetu
Katika kutekeleza maagizo
ya serikali ya kuhakikisha wasafiri wote wanaotoka katika nchi zenye maambukizi
Zaidi ya Virusi vya Corona wanatengwa, jumla ya wasafiri 84 kutoka Nchi ya Afrika Kusini
wamewekwa karantini kwa muda wa siku 14 Katika halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.
Jen. Nicodemus Mwangela ameyasema hayo alipofanya ukaguzi wa maandalizi ya
utayari wa kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe hususani maeneo ya Mipakani yaani
katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje na Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Brig. Jen. Mwangela amesema
wasafiri hao ambao ni watanzania 55 na raia wengine kutoka Congo, Afrika
Kusini, Kenya na Uganda walipoingia nchini kupitia mpaka wa Tunduma walipimwa na
kukutwa hawana dalili za virusi vya Corona na kwakuwa wametoka katika nchi
yenye maambukizi Zaidi wametengwa katika karantini.
Amesema utaratibu huo ni kwaajili
ya kuwaaangalia ndani ya siku 14 kama watakuwa hawana dalili za Ugonjwa wa
Virusi vya Corona wataruhusiwa kuendelea na safari zao.
Brig. Jen. Mwangela amewaagiza
viongozi katika sekta mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujikinga na
Virusi vya Corona pia katika ofisi na taasisi zote usafi uzingatiwe huku suala
la kunawa mikono kwa maji na sabuni liwekwe kipaumbele kila mahali.
Aidha ameliagiza jeshi la
Polisi Mkoa wa Songwe kufanya msako katika maeneno ya stendi za mabasi endapo
kutakuwa na raia kutoka katika nchi zenye maambukizi Zaidi ya Virusi vya Corona
na wamepitia njia zisizo rasmi waweze kuwekwa karantini.
Naye Kamanda wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando amesema jeshi hilo limepiga marufuku kwa
mabasi kujaza abiria kuliko uwezo wa gari, kutokuwa na vitakasa mikono kwenye
mabasi au maji na sabuni kwa ajili ya kunawa na marufuku ya mabasi kuanza
safari bila kupuliziwa dawa.
Amesema yeyote
atakayepuuzia marufuku hizo ambazo zimelenga kuweka tahadhari ya kutosambaza
ugonjwa wa Virusi vya Corona atakuwa anataka kusambaza ugonjwa kwa makusudi jambo
ambalo ni kosa kisheria hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Mganga Mkuu wa Halmashauri
ya Mji wa Tunduma Dkt Enock Mwambalaswa amesema wasafiri wote waliowekwa
karantini wanapimwa mara mbili kwa siku ili kufuatilia maendeleo ya afya zao na
endapo atatokea mwenye dalili za Virusi vya Corona hatua za haraka
zitachukuliwa lakini hadi sasa wote wanaendelea vizuri na hakuna aliyebainika
kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment