Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa
China Nchini, Wang Ke, Ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma,
Aprili 10, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mlimwa, Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana
na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Wang Ke na ameishukuru Serikali ya
nchi hiyo kwa misaada ambayo imetoa katika kukabiliana na ugonjwa wa homa ya
mapafu unaotokana na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).
“Tunaishukuru Serikali
ya China kwa misaada ambayo imetupatia hadi sasa vikiwemo dawa na vifaa tiba. Na
leo umesema kwamba kuna asasi za kiraia na wafanyabiashara bado wanakusanya
vifaa vingine ili viletwe hapa nchini vitusadie kuzuia maambukizi,
tunawashukuru sana.”
Waziri Mkuu ametoa shukrani
hizo leo (Ijumaa, Aprili 10, 2020) ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma
alipokutana na Balozi huyo. “Mchango wenu ni muhimu sana kwetu, kwa sababu tunaanza
kupata uzoefu wa namna ya kupambana na ugonjwa huu,” amesema.
Amesema Tanzania Bara na
Zanzibar zinapata wagonjwa kwa sababu ni vituo vya biashara lakini wageni wote
wanaoingia nchini kwa sasa wanawekwa sehemu maalumu ambako wanapatiwa huduma zote
wakiwa hukohuko.
“Tunashukuru Watanzania wa
pande zote mbili wanaendelea kupokea maelekezo wanayopewa, wanaendelea kujikinga
na kuchukua tahadhari za kutozunguka ovyo ili wasisambaze maambukizi,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kumshukuru Balozi wa China kwa niaba ya Serikali ya nchi hiyo kwa jinsi
ambavyo waliwahudumia wanafunzi wa Kitanzania zaidi ya 500 wanaosoma China
katika kipindi chote cha kupambana na ugonjwa huo.
“Balozi Mbelwa Kairuki
amekuwa akitupa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na jinsi mlivyowasaidia
wanafunzi wetu walioko huko na kuhakikisha wanakuwa salama tangu maambukizi yasambae
nchini China.”
“Leo hii Tanzania tumeanza
kupitia tatizo lile lile ambalo liliwapata ninyi. Tuna wagonjwa wachache lakini
tuna kundi kubwa la wale waliokutana na wagonjwa na bado tunaendelea
kuwafuatilia na kuwapima kila siku.”
“Tunaendelea na jitihada za
kuzuia maambukizi mapya, tunatoa elimu kwa wananchi wetu na kuwaelimisha kuhusu
kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono. Tunaendelea kufanya tathmini kila
siku ya watu wanaopimwa. Tumezuia mikutano na mikusanyiko yote, tumefunga shule
na vyuo, tumezuia michezo ili tusisambaze maambukizi.”
Waziri Mkuu amemweleza
Balozi huyo kwamba kwa sasa Tanzania imefunga mipaka yake kwa sababu hata nchi
jirani zimefunga mipaka yao na endapo kuna wageni wanaingia nchini, ni lazima
waende kwenye isolation centres
ambako wanalazimika kukaa kwa siku 14.
Kwa
upande wake,
Balozi Wang Ke alimfikishia salamu za shukrani Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoka
kwa Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang. “Waziri Mkuu wetu anashukuru kwa
barua ya pole uliyomtumia wakati nchi yetu inapitia janga kubwa la ugonjwa wa virusi
vya corona,” alisema.
Alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa
kwamba nchi yake sasa hivi haina maambukizi na kwamba hivi sasa wamelenga
kuzuia maambukizi mapya kutoka nje ya nchi yasiingie nchini mwao.
“Kwenye baadhi ya miji tumefungua
viwanda na vimeshaanza uzalishaji wa bidhaa ili kufufua uchumi wetu. Mwaka huu
ni muhimu sana kwetu kwa sababu nchi yetu ilijipangia kuwa uwe ni mwaka wa
kuhakikisha kuwa hakuna kabisa umaskini (zero poverty). Kwa hiyo, tunapambana
kurejesha shughuli za kiuchumi zilizoathirika kutokana na ugonjwa huu,”
alisema.
Balozi Wang Ke alisema nchi
yake imechagua baadhi ya nchi za Afrika ambazo inazisaidia kwa kubadilishana nazo
uzoefu kupitia mikutano kwa njia ya video (video conferencing) ili ziweze
kukabiliana na ugonjwa huo.
“Zaidi ya hayo, kuna misaada
ya vifaa tiba kwa ajili ya Serikali ya Zanzibar na Tanzania Bara ambayo inakusanywa
na asasi za kiraia na wafanyabiashara. Hii iko njiani, na ile ya Tanzania Bara
itawasili wiki ijayo.”
No comments:
Post a Comment