HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 15, 2020

MILIONI 416.2 ZAUNGA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA WANANCHI KATIKA SEKTA YA ELIMU NA AFYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Dkt. John Pima akitoa mada jana kwa waajiriwa wapya juu ya umuhimu wa elimu ya kujitegemea katika kuharakisha maendeleo. (Picha na Tiganya Vincent).
 
Na Tiganya Vincent

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua imetoa jumla ya shilingi milioni 416.2 ili kuunga mkono juhudi za jamii katika shughuli za maendeleo ya sekta ya elimu na afya katika mwaka huu wa fedha.

Fedha hizo zimetolewa baada ya kuona mwitiko mkubwa wa wananchi wa kuunga mkono mpango wa Halmashauri wa elimu ya kujiegemea katika kuleta maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mendaji wa Halmashauri hiyo Dkt. John Pima wakati akitoa mada kuhusu umuhimu wa elimu ya kujitegemea katika kuharakisha maendeleo katika mafunzo ya siku mbili ya waajiriwa wapya.

Alisema kati ya fedha hizo Halmashauri hiyo imenunua mabati  Bando 300 za bati kwa gharama ya  shilingi milioni  82.3, saruji mifuko 2,400 kwa  milioni 36.6 na mbao 2,072 za shilingi milioni  7.2 .

Mkurugenzi huyo Mtendaji aliongeza kuunga mkono elimu ya msingi walitoa milioni 15 na sekondari milioni 45 na katika ujenzi wa miundombinu ya afya shilingi milioni 230.

Dkt. Pima alisema baada ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kusisitiza umuhimu wa elimu ya kujitegemea kwa wananchi kumekuwepo na mwitiko mkubwa kutoka katika jamii ambao umewapelekea kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya.

Alisema katika kutambua umuhimu wa elimu ya kujiegemea ndani ya mwaka wa fedha huu wazazi katika shule za Msingi wameweza kufyatua matofali zaidi ya milioni 1.9 na kujenga vyumba vya madarasa 93, matundu ya vyoo 69 na nyumba za walimu 11.

Dkt. Pima alisema wanafunzi wameweza kulima mashamba ya mazao mbalimbali kama vile Korosho ekari 118,mahindi ekari 143, alizeti ekari 16,viazi ekari 41, Karanga ekari 80 na Mpunga ekari 23.

Alisema kwa upande wa Sekondari jamii imeweza kufyatua tofali zaidi ya laki sita na kujenga vyumba vya madarasa 56, matundu ya vyoo 36,  ya mazao ekari 121,ufugaji mbalimbali,ekari 15 za Korosho; Miti ya mbao ekari 71.8, matunda ekari 5 na mti ya vivuli miche 2,467. 

Dkt. Pima alisema katika mwaka ujao wa fedha wanatarajia kuwa na miradi ya kilimo kwa ajili ya chakula,miradi wa Kilimo kwa ajili ya biashara, upandaji miti kila shule na miradi ya matofali kila shule.

Akifunga mafunzo hayo ya siku mbili Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama aliupongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kuamua kutekeleza kwa viendo dhana ya elimu ya kujitegemea.

Alisema matokeo yake yameonyesha kuwa kupitia elimu ya kujiegemea Halmashauri zinaweza kuwa na miradi ambayo inawaingizia kipato na kuondokana na kuegemea ruzuku toka Serikali kuu.

Busalama alisema kuwa Halmashauri inaweza kujenga majengo kwa ajili ya viwanda na kupangisha wawekezaji na kupata kodi na kuondokana kutegemea zaidi kodi ya mazao.

No comments:

Post a Comment

Pages