HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 15, 2020

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA RELI YA KISASA (SGR)

 *Asema umetoa ajira zaidi ya 18,000; utapunguza muda wa safari
* Asema nguzo za umeme 154 kati ya 160 zimeshasimikwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akishuka, ndani ya treni inayotumia umeme, wakati alipokagua mradi  wa reli ya kisasa ya SGR, May 14, 2020. ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


Na Mwandishi Wetu 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kusema kuwa mradi huo umesaidia kupungua tatizo la ajira kwa kuajiri wafanyakazi 18,700.

“Kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huu, kumesaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa kutoa ajira 7,400 kwa kipande cha Dar hadi Morogoro. Kipande cha Morogoro hadi Singida kimetoa ajira 6,300 wakati mradi wa umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere nao pia umetoa ajira 5,000,” amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 14, 2020) baada ya kutembelea mradi huo na kuzungumza na wananchi aliowakuta kwenye stesheni ya Soga, iliyoko wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Amesema faida nyingine ya mradi huo katika awamu yake ya kwanza, ni kupunguzwa kwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro. Amewataka wananchi hao wawe walinzi wa mradi huo kwa sababu utakapokamilika utawanufaisha na wao pia.

Reli hiyo itakuwa na vituo sita vya Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro, huku vituo vya Dar es Salaam na Morogoro vikiwa ndiyo vituo vikuu. “Kwenye vituo vya kushusha abiria vya reli hii, kutakuwa na huduma za kibenki na maduka, kwa hiyo wananchi hata kama hamsafiri, mtaweza kupata huduma na mahitaji yenu kutokea hapo,” amesema.

Akielezea maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili, Waziri Mkuu amesema Serikali iliweka malengo ya kukamilisha mradi huo kwa wakati na ndiyo maana aliamua kwenda kuukagua.

“Katika awamu ya kwanza, ambayo inatoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km. 300), mradi huu umekamilika kwa asilimia 77.91. Hii maana yake ni kwamba wamemaliza kazi hii kwa zaidi ya robotatu. Wametengeneza njia na kulaza mataruma na mimi nimekuja na hii treni maalum kwa karibu kilometa 20,” amesema huku akishangiliwa na wananchi hao.

“Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli alianzisha mradi huu na kuwaahidi Watanzania kwamba tunaweza kuujenga kwa fedha zetu. Vilevile, mradi huu ni utekelezaji wa agizo la Ilani ya CCM ambalo linaitaka Serikali ya awamu ya tano, iimarishe usafiri wa reli nchini.”

Amesema katika kutekeleza agizo hilo, Serikali ya awamu ya tano, mbali ya kujenga reli hiyo ya kisasa, imefanikiwa pia kufufua reli ya kutoka Dar – Tanga – Moshi ambayo ilikuwa haitumiki kwa zaidi ya miaka 20. Huduma ya mizigo katika reli hiyo ilikuwa haifanyi kazi kwa miaka 12 na huduma ya kusafirisha abiria ilisitishwa tangu mwaka 1994.

Akielezea kuhusu awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa reli kutoka Morogoro hadi Makutupora, Dodoma (km. 422) ulianza mwaka jana mwishoni na sasa hivi umefikia asilimia 30 ya kazi, ambapo wanatarajia kuukamilisha ifikapo Juni, 2021.

Waziri Mkuu amesema sambamba na ujenzi wa reli hiyo, umeme pia umeanza kuwekwa ambapo nguzo 154 kati ya 160 zinazotakiwa kuwepo zimeshasimikwa. “Tumeweka miundombinu ya umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, kutoka Kidatu na Kinyerezi. Nia yetu ya kupata umeme kutoka vyanzo vyote vitatu, ni kuhakikisha kuwa umeme upo saa zote.”

“Tuna uhakika wa kutumia umeme wa Kinyerezi na Kidatu au Kidatu na Mwalimu Nyerere au Mwalimu Nyerere na Kinyerezi na hata umeme ukikatika kabisa, mabehewa yetu yana uwezo wa kutunza umeme kwa dakika 45, na katika muda huo, ni lazima tutakuwa tumerejesha umeme kutoka chanzo kimojawapo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa reli hiyo na akawapongeza mafundi wa kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki ambayo inajenga reli hiyo. “Kampuni ya Yapi Merkezi imefanya kazi kama walivyosaini kwenye mkataba na Serikali, na ninaamini watakamilisha kazi kabla ya muda,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages