Watendaji wa sekta ya ardhi katika ofisi ya Ardhi ya mkoa wa Tanga wakiwa
wamesimama katika Bango la kutambulisha ofisi ya mkoa huo.
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Ofisi
za Ardhi za mikoa kuanza rasmi kufanya kazi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara
mwezi huu wa Mei 2020 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John
Pombe Magufuli kuitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuondoa
kero na mzigo wa gharama kwa wananchi katika masuala ya ardhi.
Uanzishaji
ofisi hizo ni usogezaji huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi sambamba na kuwapunguzia
gharama za kufuata huduma hiyo umbali mrefu ambapo huduma za ardhi awali
zilikuwa zikitolewa kwenye ofisi za Ardhi za Kanda na Makao Makuu.
Akizungumza
leo tarehe 10 Mei 2020 jijini Dodoma kabla ya kuwasilisha Makadirio ya Hotuba
yake hapo kesho tarehe 11 Mei 2020, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi alisema Wizara ya Ardhi imeanzisha ofisi za ardhi katika kila Mkoa ili kutoa huduma zote
zilizokuwa zinatolewa kwenye ofisi za Kanda au Makao Makuu.
Alisema, kuanzia sasa wananchi watapata huduma zote
ndani ya mikoa yao na kubainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Kigoma na Katavi hawataenda
tena Tabora kuchukua hati kama walivyokuwa wakifanya awali huku wale wa Tanga,
Manyara na Arusha wakipata huduma katika mikoa yao badala ya kwenda Moshi na wale
wa mikoa ya Iringa, Njombe, na Rukwa wakisalia mikoa husika badala ya kwenda Mbeya.
Aidha, wananchi wa mikoa ya Ruvuma na Lindi sasa
hawataenda mkoa wa Mtwara kupata huduma za ardhi na wananchi wa Kagera na Geita
nao hawatalazimika kwenda Mwanza huku
wananchi wa mikoa ya Mara na Shinyanga wakisalia mikoa yao kupata huduma za
ardhi ambapo sasa hawataenda Simiyu na wale wa Singida na Morogoro wakiepuka kwenda
mkoa wa Dodoma kuchukua hati.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Nyaraka zote, watumishi pamoja na vitendea kazi tayari vipo
mikoani na kubainisha kuwa, sasa Taasisi kama mabenki zitaweza kukopesha kwa
kasi kwa kuwa dhamana za wakopeshwaji yaani Hati zipo mikoani na Masjala za Hati
zimerudishwa kila mkoa.
Waziri huyo mwenye dhamana ya Ardhi alisema, Wasajili
wa hati wa mikoa watatoa hati kwa wananchi kupitia ofisi za Ardhi za Wilaya na
siyo wananchi kufuata hati kwenye kanda au mkoani na kuongeza kuwa, vifaa
mbalimbali vya upimaji vimenunuliwa na kusambazwa ofisi hizo za mikoa ili
Halmashauri za Wilaya ziweze kuazima na kupima maeneo yao bila gharama za
kuvikodisha.
‘’Tumeanza mkakati wa kununua vifaa kwa kila
Wilaya. Uanzishwaji wa ofisi hizi ni
utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyetutaka Wizara
tuondoe kero na mzigo wa gharama kwa wananchi na wadau mbalimbali wa ardhi’’
alisema Lukuvi.
No comments:
Post a Comment