HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 10, 2020

SERIKALI: DAWA YA COVID 19 KUTOKA MADAGASCAR KUFANYIWA UTAFITI KWANZA KABLA YA KUTUMIWA

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema kuwa dawa ambayo nchi ya Madagascar imeitoa kama msaada wa Serikali ya Tanzania ni kwa ajili ya utafiti kwanza  kabla ya kuanza kutumiwa na walengwa. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuwa dawa hiyo inayojulikana kaitaalamu kama "COVIDORGANICS"  siyo kwa ajili ya kugawa kwa wananchi, bali ni kwa ajili ya utafiti na mara baada ya utafiti kukamilika wataalamu wa afya watatoa maelekezo ya jinsi ya utumiaji wa dawa hiyo.

Aidha, Profesa Kabudi anesema kwamba dawa hiyo imegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza la dawa ni kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya COVID 19 kwa wale ambao hawajaambukizwa ugonjwa wa Corona. Kundi la pili ni kwa ajili ya matibabu kwa wananchi ambao tayari wameathirika na COVID 19.

"Dawa hii tuliyokuja nayo jana kutoka Madagascar mara baada ya utafiti kukamilika na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wetu wa afya itatumika kukinga wananchi ambao hawajaathirika na kutibu wale walioathirika," Prof. Kabudi

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa mara baada ya kupokea dawa hiyo kazi ya kwanza ya ni kuanza utafiti ambao utaonesha kama dawa hiyo ni salama na haina madara kwa wananchi na pili utafiti wa kuangalia ubora wa kutibu au kupunguza makali ya COVID 19.

"Mara baada ya utafiti wa dawa hii kukamilika itatumika katika makundi matatu ambayo kundi la kwanza ni wagonjwa kutumia dawa ya kawaida, kundi la pili watapata dawa ya kawaida na hii iliyotoka Madagascar na kundi la tatu wagonjwa watatumia dawa ya kawaida na ile inayozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr)," Amesema Prof. Makubi

Prof. Makubi pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa watanzania kuchukua tahadhari katika kujikinga na ugonjwa wa COVID 19 na wasibweteke na lolote.

Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Yunus Mgaya amesema kuwa wamejipanga kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali hasa Ofisi ya Mkemia Mkuu katika kuhakikisha inafanya utafiti wa kina juu ya matumizi ya dawa hiyo.

"NIMR inafanya tafiti mbalimbali za kupambana na ugonjwa huu wa COVID 19 na itaendelea kufanya tafiti hizo ili kuwasaidia watanzania," amesema Prof. Mgaya

Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu inalo jukumu la kuchunguza dawa au sumu zozote kwenye sampuli, kukadiria kwa usahihi kiasi cha dawa, umetaboli au sumu.

Dkt. Mafumiko ameongeza kuwa, kupitia utafiti wa dawa hiyo, ofissi yake kwa kushirikiana na wataalamu wa afya watatafsiri matokeo ya uchunguzi katika dawa hiyo kutoa maelekezo sahihi juu ya matumizi yake kwa mwananchi.

Mkutano huu ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Tiba za Asili Dkt. Paul Mkama.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha JNICC jijini Dar  leo, mara Baada ya kurejea kutoka nchini Madagascar kuchukua dawa ya virusi vya Corona, ii kupambana na maradhi hayo ya COVID – 19 ambapo itafanyiwa utafiti kabla ya kuanza kutumiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages