HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 02, 2020

VIONGOZI WA DINI WATOA TAHADHARI KUJIKINGA NA CORONA

Alodia Dominick, Karagwe

Viongozi wa madhehebu ya dini ya kikristo na kiislamu wilayani Karagwe wametoa wito kwa wananchi wilayani humo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya kujikinga na virusi vinavyosababisha corona kwani virus hivyo vina ua na havina dawa wala tiba.

Viongozi hao wametoa wito huo wakiwa ofisi za halmashauri ya wilaya ya Karagwe baada ya familia ya sir Goerge Kahama kukabidhi vifaa mbalimbali ambavyo vitasaidia wananchi katika kujikinga na virus hivyo.

"Janga hili siyo la mchezo Tanzania tuna mahali pa kutazama baada ya nchi nyingine ugonjwa ulipoanzia walivyoathirika na kupoteza wananchi wao wengi hivyo kila mwananchi atumie silaha yake katika kujiwekea tahadhari bila kupuuza maagizo ya wataalamu" Alisema Dr Benson Bagonza Askofu wa KKKT dayosisi ya Karagwe.

Bagonza ameongeza kwa sasa dayosisi yake wamesitisha ibada kwa wiki 4 na kuwa kama kanisa wanajiweka tayari kwa kuandaa vifaa mbalimbali kama barakoa na vitakasa mikono ili ibada zitakapofunguliwa wananchi wawe na vifaa vya kujikinga kanisani.

Shehe wa wilaya ya Karagwe Nassibu Abdul amesema, katika misikiti wameendelea kuelimisha waumini wao na kuwasisitiza  kunawa mikono na kuvaa barakoa ili wajikingine lakini pia wawalinde watoto wao wasiwaruhusu kuzurula ovyo wakae nyumbani kwani lengo la serikali kuwarudisha nyumbani lilikuwa kuwakinga na virus vya corona.

Mwakilishi wa Askofu wa kanisa la Roman catholiki jimbo la Kayanga padre Hans Humma amesema kanisa ni kama hospitali ya kiroho hivyo wataendelea kutoa elimu kwa waumini wao kupitia ibada na hawatafunga kanisa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Godwini Kitoka ametaja msaada wa vitu vilivyotolewa kuwa ni pamoja na ndoo za kok 240, sabuni za maji 240, vipaza sauti nane vya kutolea elimu na mashine mbili za kupima joto vyenye thamani ya shilingi 7.5 milioni.

Aidha Janeth Dina Kahama mke wa marehemu sir Goerge Kahama amesema kama familia wamewiwa kutoa vifaa hivyo kwa halmashauri ili visaidie katika janga ambalo limekuwa tishio kwa dunia nzima na aliwaomba wadau wengine kujitokeza katika kutoa misaada mbalimbali itakayosaidia wananchi kujikinga na virus vya corona.

No comments:

Post a Comment

Pages