HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 21, 2020

Wafanyabiashara walalamikia ‘nyaya’ zisizo na ubora katika soko

WAFANYABIASHARA wa vifaa mbalimbali vya umeme jijini Dar es Salaam  wamelalamikia uwepo wa vifaa hivyo hususani nyaya zisizo na ubora zinazozalishwa na baadhi ya viwanda hapa nchini na kuiomba Serikali kupitia Shirika la viwango Tanzania (TBS) na tume ya ushindani (FCC) kufanya msako viwandani na madukani ili kuwabaini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kariakoo, baadhi ya wafanyabiashara hao pamoja na wanunuzi wa bidhaa hizo wamedai kumekuwepo na wimbi la uzalishaji wa bidhaa hizo hususani nyaya za umeme za majumbani ‘wiring’ zisizo na viwango  unaohitajika.
Wafanyabiashara hayo waliojitambulisha kwa majina ya Rashid Salum pamoja na Frank Mtonga waliopo eneo hilo, walisema kumekuwepo na bidhaa hizo katika baadhi ya maduka ya kariakoo na hivyo kusababisha maduka yanayouza bidhaa zenye viwango bora kukosa wateja kutokana na wananchi wengi kukimbia kwa kigezo cha bei na kuzifuata nyaya zisizo na ubora kutokana na unafuu wa bei bila kujua athari zake.
“Kuna maduka mengi hasa maeneo ya mitaa ya Narungombe na maeneo mengine yanye maduka yanayouza bidhaa hiyo, wanauza nyaya ambazo hata ukizitamaza kwa macho utabaini kuwa hazina ubora, kigezo kikubwa kinachofanya wananchi wazikimbile ni unafuu wa bei” alisema Salum
Bila kutaja majina ya viwanda vinavyotengeneza nyaya hizo,Salum alisema kimsingi nyaya hizo pamoja na baadhi ya vifaa vingine vya umeme, vinazalishwa kutoka katika viwanda vinavyomilikiwa na raia wa kigeni wasio waaminifu na kuiomba Serikali kufuatilia kwa undani ili kubaini.
Kwa upande wake Mtonga alisema yeye kama mfanyabiashara aliwahi kupokea lawama kutoka kwa baadhi ya wateja wake, waliomtuhumu kuwauzia nyaya zisizo na ubora, suala alilodai kuwa hakulifahamu kwa kuwa hakuwa na uelewa wa kutosha juu ya nyaya hizo na viwango vyake.
Aliiomba TBS kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka pamoja na viwandani  hatua itakayosaidia kuwabaini wahusika kisha kuchukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu za nchi kwa madai kuwa wengi wa wenye viwanda hivyo wamekuwa wakifanya hayo kwa makusudi licha ya kujua athari za kufanya hivyo.
Akitolea mfano katika suala hilo, Mtonga alisema kwa nyaya zenye ubora wa viwango ambazo zinauzwa kwa wastani wa Sh 100,000, huuzwa kwa wastani wa hadi 70,000 kwa nyaya zisizokuwa na ubora wa viwango na hivyo kuathiri ushindani wa bei katika sokoo huku pia zikileta madhara kwa wananchi yakiwemo ya nyumba kuungua.
Alisema athari nyingine inayoweza kusababishwa na kuzalishwa kwa nyaya hizo zisizo na ubora ni pamoja na kuwaweka katika wakati mgumu wao kama wauzaji wa reja reja pindi watakapobainika na Serikali kuuza bidhaa hizo kutokana na kuwa suala hilo ni kinyume cha sheria.
“Tunawaomba TBS pamoja FCC kuendesha ukaguzi wao wa mara kwa mara katika maduka yanaouza bidhaa za umeme lakini pamoja huko kwenye viwanda zinapozalishwa ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika kama njia moja wapo ya kukomesha biashara hiyo”
Kwa nyakati tofauti Serikali kupitia Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani imekuwa ikisisitiza utumiaji wa vifaa vya umeme vyenye ubora vinavyozalishwa hapa nchini na kupiga marufuku uzalishaji wa vifaa vyote visivyo na ubora, agizo linaloonekana kupuuziwa na baadhi  ya wenye viwanda hivyo.

No comments:

Post a Comment

Pages