HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 18, 2020

Women Fund Tanzania Trust wafanya uchambuzi wa sheria tano za uchaguzi

Mwenyekiti wa WFT, Profesa Ruth Meena. (Picha ya Mkatba).


Na Janeth Jovin

MTANDAO  wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi chini ya uratibu wa Mfuko wa Udhamini wa  Wanawake Tanzania ( Women Fund Tanzania-Trust ) ,wamefanya uchambuzi wa sheria tano za uchaguzi kwa mrengo wa jinsia ili kutoa muhtasari wa mambo yaliyojitokeza kwenye baadhi ya Sheria za Uchaguzi.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa WFT, Profesa Ruth Meena  kwa njia ya mtandao na wanahabari alisema  uchambuzi huo utaweza kubainisha mapengo  yanayoweza kuwa kikwazo katika kutekeleza azma ya ujenzi wa demokrasia shirikishi kwa mrengo wa jinsia na kutoa  mapendekezo mahususi yatakayoongoza wadau mbalimbali katika kuchukua hatua stahiki zenye kukabiliana na sheria za ubaguzi wa aina zote hususani ubaguzi wa jinsia kwenye mchakato wa uchaguzi.

Alisema Sheria zilizochambuliwa ni pamoja na Sheria ya  Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ya 2015,Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 4  (2018), Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa namba 4 ya mwaka 1979 s namba 292 kama ilivofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na mwaka 2015),Sheria ya  Serikali Za Mitaa ( Mamlaka za Wilaya Sura 287 kama ilivyorekebishwa 2002) na Sheria za Serikali za Mitaa za mmlaka za miji sura ya 288 na mamlaka za wilaya sura ya 287.

 “ Lengo la Mkutano huu ni kuwezesha wanahabari kupata taarifa za kina zilizotokana na uchambuzi wa sheria zilizochambuliwa kwa mrengo wa Jinsia. Kimantiki, wanahabari ni muhimu sana kwenye ujenzi wa demokrasia shirikishi na kwenye harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi,"alisema na kuongwza kuwa

“ Wanahabari  ni kiungo  kinachounganisha  jamii, wanaowania kuomba dhamana ya uongozi kwa wapiga kura au kuwasilisha madai ya wapiga kura kwa wale wanowania kuomba dhamana ya uongozi.” aliongeza Prof.Meena

Pro. Meena alieleza mambo yalibainishwa mara baada ya kuchambuliwa kwa sheria hizo tano  ni pamoja na mfumo wa uchaguzi unaongozwa na dhana ya “MSHINDI ANAPATA YOTE” yaani “the winner gets all” hauko rafiki kwenye uwakilishi wa makundi yote na demokrasia shirikishi.

Alisema  takwimu toka nchi nyingi zinazotumia mfumo huo zinaonyesha kwamba ufikiaji wa azma ya usawa wa jinsia ni mgumu.

Pia kwenye suala la haki ya kupiga kura ambapo alisema katiba zote mbili ya Tanzania bara na visiwani zinabainisha haki sawa ya kupiga kura kwa raia wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea

Akitoa Mfano Prof. Meena alisema  takribani asilimia 95 ya wapiga kura waliojiandikisha mwaka 2015 katika Uchaguzi mkuu takribani ya wanawake waliopiga kura  walikuwa asilimia 53 ya wapiga kura wote kwa mwaka huo na hiyo inaonyesha kuwepo kwa  ongezeko la wanawake waliojiandikisha kupiga kura kwenye Uchaguzi huu wa mwaka  2015 kwa asili mia 4.4  ya wale waliojiandikisha katika Uchaguzi wa mwaka 2010.

Akizungumzia haki ya Kuteuliwa alisema  uteuzi wa Wagombea ni msingi wa kupata wagombea wenye sifa na hatimaye viongozi bora.

"Mapungufu yaliyopo ni kuwa wagombea wote, kwenye mchakato wa uchaguzi, lazima wawe ni wanachama wa vyama vya siasa na wawe wamependekezwa na vyama husika  Kifungu cha 26 (2) (d) cha Katiba ya Zanzibar – 2018 na kifungu cha 36 cha Katiba ya Jamhuri (1977) imehainisha hayo," alisema na kuongeza
"Muktadha unaoongozwa na mfumo dume ndani ya vyama vya siasa na uongozi usio na utashi wa kuzingatia usawa wa jinsia uwaumiza   wanawake zaidi... Takwimu za chaguzi zote zinaonesha jinsi vyama vinavyobagua wanawake kwenye uteuzi  Mfano mwaka 2015  asilimia ya  wagombea viti vya ubunge (Wanawake) ilikua  Chama cha ACT- Wazalendo ilikuwa  15, CUF asilimia 11, CCM asilimia 9 na CHADEMA  asilimia 6," alisema Prof.Meena

Alisema hali ya ushiriki huo katika uchaguzi wa mwaka 2015 inaonesha kutokuwepo na utashi wa siasa wa kutekeleza azma ya ujenzi wa demokrasia shirikishi kwa mrengo wa jinsia.

Prof.Meena alisema sheria ziko kimya kwenye kuwajibisha vyama vinavyokiuka sharti la usawa wa jinsia katika uteuzi wa wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi.

***Akizungumzia suala la gharama  za uchaguzi ,Sheria zinatoa sharti la kuweka dhamana ya kiwango fulani cha pesa kwa wagombea, kwa mfano kiwango cha Sh.Milioni moja kwa Rais wa  Tanzania na Million Mbili kwa mgombea kiti cha Urais Zanzibar.

Alisema Viwango hivyo alivieleza na kuwa ni kikwazo cha wanawake wenye uwezo wa uongozi, lakini hawana uwezo wa kifedha.


***Akizungumzia suala la Uwajibikaji

Sheria haijatoa meno kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwajibisha vyama vya siasa, ambavyo kwenye uteuzi, hawazingatii usawa wa jinsia kwenye uteuzi wao.

Akizungumzia Suala la viti Maalum
Azma ya kuwepo kwa Viti Maalum imetumiwa kwa njia iliyoingiza ubaguzi kati ya wajumbe wa kuchaguliwa majimboni na wale wanaoingia Bungeni kwa kuteuliwa Viti Maalum. Mbunge wa Viti Maalum hawezi kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu, hapewi fedha za jimbo (kwa ajili hawakilishi jimbo) na hubaguliwa kuingia kwenye kamati mbalimbali za Bunge. Kuna haja ya kuboresha Sheria za Viti Maalum ambavyo kimsingi hupewa wanawake.

Akizungumzia juu ya Vyombo vya habari  Prof.Meena  alisema Wanahabari wanapaswa kujielimisha kuhusu masuala ya jinsia katika mchakato wote wa uchaguzi ili kubaini mapengo ya utekelezwaji wa sheria za uchaguzi kwa mrengo wa jinsia. Maarifa haya yatawapa wanahabari nyenzo ya kutetea haki ya ushiriki wa wanawake katika mchakato wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

Pages