Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Mweri Kilimali, akizungumza na waandishi wa habari.
Mkuu
wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Mweri Kilimali (kushoto), akimkabidhi mali
yake Tarimo Kakiza baada ya kuchukuliwa na wakopeshaji wanaotoa mikopo
Umiza.
NA DENIS MLOWE, IRINGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambanana na Rushwa mkoa wa Iringa,
kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imemfikisha Mahakamani aliyekuwa
Rais wa Wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha (CDTI) Christopher
Mollel kwa makosa manne.
Akizungumza na wanahabari mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa,
Mweri Kilimali alisema kuwa makosa ambayo yamemfikisha mahakamani Mollel ni kosa
la wizi wa sh. Milioni 1,250,000 kinyume na kifungu cha 258(1) kikisomwa pamoja
na kifungu cha 265 vya sheria ya kanuni ya adhabu ya sura ya 16 pitio la mwaka
2002.
Kilimali alisema kuwa kosa jingine linalomkabili Christoher
Mollel ni kugushi kinyume na vifungu vya 333,335(d) (1) na 337 vya sheria ya
kanuni ya adhabu sura ya 16 pitio la mwaka 2002 na kosa jingine ni kuwasilisha
maelezo ya uwongo kinyume na kifungu cha 342 kikisomwa pamoja na kifungu cha
337 vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 pitio la mwaka 2002 pamoja.
Aidha alisema kuwa kosa jingine linalompandisha kizimbani ni
kosa la kutoa taarifa ya uwongo kwa mtu aliyeajiriwa katika mamlaka ya Umma
kinyume na kifungu cha 122(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 pitio
la mwaka 2002.
Alisema kuwa makosa hayo yametokana na Takukuru mkoa wa
Iringa kubaini kuwa mnamo Oktoba 25 mwaka 2019 mtuhumiwa akiwa Rais wa serikali
ya wanafunzi wa chuo hicho alichana na kuiba hundi namba 000063 kutoka katika
kitabu cha hundi ya Ruaha CDTI Student Organization kilichokuwa kimehifadhiwa
ofisini kwa mshauri wa wanafunzi wa chuo hicho.
“Baada ya kuiba hundi hiyo alijaza taarifa za uongo za
kutakiwa kulipwa fedha kiasi cha sh. 1.250,000 ambapo alisaini akiwa mmoja wa
watia saini katika akaunti hiyo na kughushi saini ya mtia saini (Mwalimu) wa
Pili katika akaunti hiyo” alisema
Aliongeza kuwa uchunguzi ulibaini kuwa mtuhumiwa Oktoba 26 mwaka 2019 aliwasilisha hundi hiyo
namba 000063 ya akaunti 60510007147 katika benki ya NMB tawi la Mkwawa iliyopo
Iringa Mjini akiwa ameambatanisha na nakala ya kuwekea Hundi ambayo ilikuwa na
maelezo ya kutoa fedha kiasi hicho kutoka akaunti ya Ruaha Cdti student
Organization kwenda kwenye akaunti yake binafsi namba 6051.
Kamanda Kilimali alisema kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo
umekamilika na mtuhumiwa amepandishwa mahakamani leo katika mahakama ya wilaya
ya Iringa.
Alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kutofumbia macho
wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuwataka wananchi kutoa taarifa sahihi
kwa tukukuru ili hatua stahiki zichukuliwe kwa yoyote anayevunja sheria hasa
katika masuala ya rushwa.
No comments:
Post a Comment