HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 30, 2020

Benki ya NMB yahimiza matumizi ya Bima

BENKI ya NMB imewashauri wafanyabiashara kutumia huduma mbalimbali za bima zinazotolewa na benki hiyo kulinda biashara zao pamoja na mali nyingine ili kujikinga na majanga anuai yanayoweza kurudisha nyuma biashara. 

Kauli hiyo imetolewa na, Meneja Mwandamizi wa Bima Benki ya NMB, Martine Massawe jijini Arusha alipokuwa akiwatembelea wafanyabiashara mbalimbali pamoja na kukabidhi nyaraka za bima kwa baadhi waliojiunga na huduma za bima.

Alisema bima kwa mfanyabiashara ni muhimu sana kwani inamfanya aweze kufanya biashara yake kwa kujiamini, kwani hata kama itapatwa na majanga kama ya uhalifu, moto au maafa mengine mteja atasaidiwa na biashara kurejea kama awali.

Aidha aliongeza Benki ya NMB kwa kutambua umuhimu wa huduma za bima kwa wateja wake sasa inauwezo wa kumkopesha mteja ili afanikiwe kukata bima kisha mteja kurejesha taratibu huku biashara yake ikiwa salama muda wote.

"Sasa hivi mteja mwenye sifa tunaweza kumkopesha fedha kisha akakata huduma ya bima aitakayo kulingana na mahitaji yake, na mkopo huo ataulipa taratibu huku tayari biashara yake ikiwa salama, tunatambua usalama wa biashara ya mteja wetu ni jambo la msingi," alisema Massawe.

Hata hivyo alishauri Watanzania wote kujenga utamaduni wa kukata bima mbalimbali ili kujikinga na majanga ambayo yamekuwa yakiwarudisha nyuma kiuchumi pindi yanapotokea.

Alisema kwa sasa Benki ya NMB imemsogezea mwananchi karibu huduma zote za bima ili aweze kujikinga dhidi ya majanga kama vile uhalifu, bima ya kilimo, chombo cha moto, maisha, mali yoyote, elimu na afya kupitia matawi yote ya benki hiyo.

Benki ya NMB imeanza kutoa huduma za bima katika matawi yake yote nchini mara baada ya kuzinduwa huduma ya bima kupitia benki (Bancassurance) uliofanyika hivi karibuni jiji Dar es Salaam.

Huduma za bima zitakazopatikana katika matawi ya Benki ya NMB ni pamoja na zile za kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (National Insurance Corporation - NIC), Jubilee, Shirika la Bima la Zanzibar na Reliance.
Ofisa wa Benki ya NMB Tawi la Clock Tower mkoani Arusha, Mussa Lumala (kushoto), akimkabidhi nyaraka za bima mmoja wa wateja katika benki hiyo mara baada ya kukata leo tawini hapo. Benki ya NMB inaendeleza kampeni yakuhamashisha watanzania kupata bima lengo likiwa kuhakikisha kuwa asilimia 60 ya Watanzania watu wazima wawe wanapata huduma za bima ifikapo mwaka 2024.

No comments:

Post a Comment

Pages