Mama
mzazi wa aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga, akipita
kuaga mwili wa mwanaye wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika Juni 3,
2020 kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Tom Apson akiweka
udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga
wakati wa mazishi yaliyofanyika Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia
kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Alhaj Yusuf Mfinanga ambaye ni baba mdogo wa marehemu Christopher Mfinanga aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu akiweka udongo kwenye kaburi lake wakati wa mazishi yaliyofanyika katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Jeneza lenye mwili wa Christopher Mfinanga
likiwa kaburini wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi
ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Padre Japhet Njaule wa parokia ya Vuchama akipanda
msalaba kweye kaburi la aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga
wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya
familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Mama mzazi wa Christopher
Mfinanga akiweka shada la maua wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3,
2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Wachungaji na Padri walioshirikiana kuongoza
ibada ya mazishi ya aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga
wakichukua udongo ili wauweke kaburini kwenye mazishi yaliyofanyika jana Juni 3,
2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Wachungaji na Padri walioshirikiana kuongoza
ibada ya mazishi ya aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga
wakichukua udongo ili wauweke kaburini kwenye mazishi yaliyofanyika jana Juni 3,
2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Mchungaji Bill Grahama Msangi wa KKKT
Usharika wa Vuchama akihitimisha ibada ya mazishi ya aliyekuwa mpigapicha wa
Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni
3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.
Makaburi mawili, moja la Baba na jingine la mwana. Kulia mbele ni kaburi la
aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga na la kushoto ni
la Baba yake Mzee Edward Dologha Mfinanga aliyefariki jijini Arusha Mei 19,
2020 na kuzikwa Mei 21, 2020 kijijini kwake Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga.Na Mwandiushi Wetu, Mwanga
MKUU wa Wilaya ya Mwanga,
Bw. Tom Apson ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw.
Chris Mfinanga yaliyofanyika kwenya kijiji cha Mangio, Vuchama, wilayani humo.
Akizungumza na waombolezaji kijijini
hapo jana (Jumatano, Juni 3, 2020), Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alimwakilisha
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Anna Mgwira alisema Chris Mfinanga alikuwa
mtu aliyejaa upendo ndiyo maana wengi wanahuzunishwa na kifo chake.
“Chris alikuwa mtu mcheshi na
mwenye upendo, alisaidia wengi lakini tusisahau kwamba Mungu ndiye mtoa riziki.
Msikate tamaa kwa sababu Mungu yupo na alimwezesha Chris na ndiyo maana aliweza
kuwasaidia wengine na hata kuwasomesha watoto wenu.”
“Ninawasihi muamini kuwa Yesu
yupo na kwake kuna faraja. Amini Yesu yupo na usiamini katika mganga wa
kienyeji au ushirikina. Tuache ramli, tumtegemee Mungu nasi tutapata faraja,” alisisitiza.
Mapema, akiongoza ibada hiyo, Mchungaji
Kiongozi wa KKKT Usharika wa Vuchama, Bill Graham Msangi aliwataka waombolezaji
waweke mambo yao sawa na Mungu wao pamoja na majirani wanaoishi nao.
Akitoa mahubiri kutoka
kitabu cha Ufunuo wa Yohana (14:13), Mchungaji Msangi alisema watu wanaomwamini
Kristo wana heri kwa sababu wanapoaga dunia ni sawa na watu wanaoenda kupumzika
baada ya taabu zao hapa duniani. “Wanaokufa katika Bwana wanaenda kupumzika
baada ya taabu zao. Wana heri sababu matendo yao yanafuatana nao.”
“Kama wewe ni mchawi au
mpiga ramli na kazi yako ni kuchonganisha watu, au wewe ni kibaka au mfitini,
je hayo matendo yako utaenda nayo wapi? Kule kwenye pumziko siyo kwao watu wa
aina hiyo,” alisema.
“Neno la Mungu limesema;
bali wao wasioamini, waongo wote, wachukiao na wezi wote na waabuduo sanamu,
sehemu yao ni kwenye ziwa la moto ambao hata mende hawaungui. Hata uwe tajiri kiasi
gani, au uwe mzuri kiasi gani au uwe baunsa, hautaweza kuzuia kuingia kwenye
jehanamu ya moto eti kwa sababu ya ubaunsa wako.”
“Tunapaswa tujiandae kwa sababu
siku ikifika, Mungu haatangalia uzuri ulionao. Yeye Mungu ni mzuri kuliko huo uzuri
wako. Shetani alikuwa mzuri sana lakini alipoasi alifukuzwa.”
Aliwasihi wafiwa na wakazi
wa kijiji hicho hao wawe na umoja ili amani iweze kutawala. “Umoja ukae miongoni mwa familia, ukae miongoni
mwa kaya nyingine na wanavijiji wote. Tukiishi kwa namna hiyo, amani itatawala
kwa sehemu kubwa.”
Naye Padre Japhet Njaule wa
Parokia ya Vuchama ambaye aliongoza mazishi ya Baba yake Chris Mei 21, 2020,
aliwataka waombolezaji wamtumaini Mungu na waishi kwa kujiandaa na kuwa tayari
wakati wote.
“Sisi sote ni mali ya Bwana.
Tuishi leo na sasa kana kwamba ni saa hii tunaondoka na wala tusiwaze kuhusu
kesho yetu. Tukumbuke kuwa Mungu ana mpango na maisha ya kila mmoja wetu,”
alisisitiza.
Akizungumza
kwa niaba
ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Fadhili Liwaka aliwataka wanafamilia wapate faraja
kutoka kwa Mung una wala wasiumizwe na msiba wa Chris. “Tusione ajabu ya msiba
huu kwa sababu hili ni jaribu la moto na Mungu anatukumbusha juu ya kuzaliwa,
kuishi na kufa. Hakuna binadamu ambaye anaweza kukwepa kifo na hakuna mahali
mapenzi ya mwanadamu yanaweza kuzuia kifo cha yule unayempenda.”
Alisema: “Msiba unapotokea,
unatukumbusha kuwa tutarejea kwa Mungu, pia utakuja kutuunganisha kama ndugu na
kutujulisha kuwa hii neema ya Mungu na si jambo la kibinadamu na tatu
unatukumbusha juu ya kujenga, amani, utulivu na kukubaliana na matokeo.”
Naye Baba mdogo wa marehemu,
Alhaj Mzee Yusufu Mfinanga aliwashukuru madaktari na wauguzi waliomhudumia
Chris wakati akipatiwa matibabu. Pia aliwashukuru ndugu, jamaa, marafiki, majirani
na wafanyakazi wenzake kwa ushirikiano mkubwa waliounesha. “Ushirikiano huo ni
dalili tosha kwamba Chris alikuwa akiishi vizuri na watu.”
No comments:
Post a Comment