Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo ameusifu uongozi wa Wilaya ya Nkasi unaongozwa na Mkuu wa Wilaya
hiyo Mh. Said Mtanda pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Nkasi Missana Kwangura kwa kutekeleza maagizo ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh Suleiman Jafo kwa wakati na kwa ufanisi
mkubwa na hatimae wananchi wameanza kupata huduma katika hospitali ya Wilaya
hiyo.
Wakati akitoa pongezi
hizo Mh. Wangabo alisema kuwa hivi karibuni tarehe 2.6.2020 Mh. Jafo alifanya
ziara katika Wilaya ya Sumbawanga na kuzitaka hospitali mpya 67 za Wilaya
nchini kuanza kufanya kazi kuanzia tarehe 8.6.2020. ili kufikia lengo
lililotarajiwa la kuwasaidia wananchi kupata huduma za kiafya katika ngazi ya
Wilaya.
Aidha, Mh. Wangabo
alisema kuwa serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeongeza Shilingi
bilioni 1.4 kwa hospitali tatu za Wilaya ambapo kila hospitali imepatiwa
shilingi milioni 300 kwaajili ya kuelekezwa kwenye maeneo ambayo yanatakiwa
kukamilishwa katika ujenzi wa hospitali hizo wakati Halmashauri ya Manispaa ya
Sumbawanga imepatiwa Shilingi Milioni 500 kwaajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali
mpya ya Manispaa hiyo.
“Nilipokuwa naingia
tu imenishangaza, yaani nilifikiri imeanza kutumika miezi sita iliyopita,
lakini ni ndani ya wiki moja, mazingira haya yameboreshwa namna hii na kila
kitu kipo kwenye mpangilio wake, tunastahili kupongezana, lakini pongezi za
aina yake ziende kwa uongozi wa wilaya hii ya Nkasi, Mheshimiwa DC tumpigie makofi,
amesimamia vizuri san ana anaendelea kusimamia vizuri sana, Wilaya yake, lakini
Siwezi kuacha kumpongeza sana Mkurugenzi wetu wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,”
Alisema.
“Jambo jingine ambalo
ningependa wananchi mfahamu, Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli ametoa
tena shilingi bilioni 1.4 katika mkoa wetu wa Rukwa, Kila hospitali ya Wilaya
katika zile tatu, zitapata milioni 300 na tayari fedha hizi zipo, Rais wetu Dkt.
Hohn Pombe magufuli anatupenda sana, na fedha hizi ni lazima zitumike ndani ya
mwezi huu kabla ya mwaka wa fedha haujaisha, Mkurugenzi wa Nkasi hakikisha
kwamba milioni 300 zinaelekezwa kwenye maeneo yale ambayo yametakiwa kuelekezwa,”
Alisisitiza.
Pia aliwaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha maeneo yote ya hospitali hizo yanapimwa
na kupatiwa hati haraka iwezekanavyo ili kuepusha migogoro na wananchi ambao
wanazunguka maeneo hayo kwa kufanya shughuli za kilimo.
Awali akisoma taarifa
ya uzinduzi wa huduma za afya katika hospitali ya Wilaya ya Nkasi Mganga Mkuu
wa Wilaya hiyo Dkt Hashim Mvogogo alisema kuwa huduma ambazo zimeanza kutolewa katika
hospitali hiyo ni pamoja na wagonjwa wa nje (OPD), Meno (Dental Clinic), Macho
(Eye Clinic), Kujifungua, Kliniki ya Wajawazito na Watoto na huduma ya Maabara.
“Jumla ya Watumishi
28 tumewabadilisha kutoka katika vituo mbalimbali na kuwaweka katika hospitali
hii ambayo tunaifungua leo (8.6.2020), aidha, dawa na vifaa tiba tumefanya ‘re-allocation’
kutoka katika vituo mbalimbali ndani ya Wilaya yetu ili kuhakikisha kuwa huduma
hii tunaweza kuitoa,” Alieleza.
Kwa upnde wake Mganga
mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa baada tu ya kupokea
maagizo kutoka kwa Mh. Jafo, Katibu Tawala Mkoa aliteua wataalamu wachache
kutoka ngazi ya Mkoa akiwemo Mganga Mkuu huyo kwaajili ya kuratibu utekelezaji
wa maagizo hayo na kuifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa halmashauri
pamoja na timu za afya ngazi za wilaya.
“Na kwa watumishi
ninavyowaona naona huduma hasa za OPD zimeanza kama ilivyoagizwa, tulielekezwa
kuanza na huduma za awali, kwa maana ya huduma za wagonjwa wa nje lakini ikiwezekana
huduma za wazazi, kama ulivyosikia kwenye taarifa, lakini baada ya muda mfupo
ujao tunategemea hospitali yetu ianze kutoa huduma zote,” Alisema.
Kwa upande mwingine,
Mh. Wangabo alitembelea hospitali ya Wilaya ya Kalambo ambayo hakurudhishwa na
mazingira aliyoyakuta baada ya hospitali hiyo kukamilika kwa asilimia 76 huku
maeneo mengi yakihitaji kumaliziwa ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment