WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa (pichani), amesema idadi ya wananchi waliojiandikisha
kupiga kura imeongezeka ambapo wapiga kura halali kwa mwaka huu ni 29,804,992
ikilinganishwa na wapiga kura 23,161,440 wa mwaka 2015.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amesema Tume inaendelea na uchambuzi wa taarifa za wapiga kura
waliojiandikisha na baada ya zoezi hilo kukamilika, Daftari la mwisho
litakalotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 litaandaliwa na kuwekwa wazi.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati
akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, ambapo amesema kwa sasa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi inaendelea vema na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Amesema takwimu
za awamu ya kwanza na ya pili, zinaonesha kuwa wapiga kura wapya
walioandikishwa ni 7,326,552, wapiga kura walioboresha taarifa zao ni 3,548,846
na wapiga kura 30,487 wamepoteza sifa.
Amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura wa awamu ya kwanza lilianza rasmi Julai 18, 2019 na kukamilika Februari 23,
2020 kwa nchi nzima wakati awamu ya pili ilianza Aprili 17, 2020 na kukamilika
Mei 5, 2020.
“Hivi sasa, pamoja na mambo mengine Tume imekamilisha
matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kufanya Uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na mwingine.”
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi
wazingatie Katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa
shughuli za uchaguzi.
Vilevile, Waziri Mkuu amewasihi viongozi na wanachama wa
vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla waendelee kulinda amani na
kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment